NITAKUUA MWENYEWE - 44 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 44

sultanuwezotz.blogspot.com 


    Baada ya mwendo mrefu Roberto aliwasili kwenye Ngome ya Santana maeneo ya msitu wa San Antonio ulio karibu na Ufukwe wa Marigezh na msitu huu ndani yake kuna msitu mwingine wa kupandwa ambao ulipandwa na mzee Tuyilagezi aliyekuwa zungu la Unga kwa wakati huo kabla ya kuuawa na Santana uitwao Caratons na ndani yake mzee huyu alijenga jumba lake la kifahari ambalo ukiwa ndani ya kisiwa cha Marigezh utaliona vizuri jumba hilo lillilo kwenye miamba na hivyo Santana hukitumia kwenye masuala yake na wageni ambao huwa hataki wajue anafanya nini. Na kwa kuwa analifahamu vizuri eneo hilo halikuwa tatizo kwake ni wapi apitie ili kuingia ndani ya Ngome hiyo. Lakini wakati akijipanga aingilie Ufukweni Marigezh au Caratons aliisikia gari ikitoka ndani ya Ngome ikabidi ajifiche kwenye kichaka asije onwa na wenyewe, mara ile gari ilisimama karibu na pale alipojificha kisha mtu mmoja ambaye hakumfahamu vizuri aliteremka akawa anakagua mazingira kisha mlango wa pili ulifunguliwa na Santana aliteremka. 

"Hebu nisubirini kwanza nimekumbuka kule ndani kuna vitu ambavyo ni kumbukumbu za wale mizoga na kama ambavyo niliahidi kuwa sihitaji chochote cha kuwakumbuka."

Santana aliongea akimpiga bega Robinson ambaye alimfanya kama mlinzi wake wa muda wakati anamuandalia programu. 

" Ni vitu gani hivyo mkuu?" Robinson alimuuliza. 

" Si zile simu zenu ambazo niliwaambia kipindi kile mziache kwa mwezi mmoja."

"Okay, kwanza nilikuwa nimeshazisahau mkuu." 

"Kimbia ndani mwambie Melissa aingie ofisini kwangu kwenye droo ya meza yangu aangalie ataona bahasha ya kaki akupe ulete hapa." Aliagiza huku yeye akijivuta kwenye kiti kiti cha gari mlango ukiwa wazi. 

"Sawa bosi." Robinson aliitikia na kuondoka haraka kurudi ndani. 

"Unajua nini Chude kitendo cha wanaharamu wale kufa na kutupwa baharini nimekuwa na amani sana moyoni na ni imani yangu kwa sasa yamebakia maskeletoni tu." 

"Ni kweli bosi ila mimi bado nina hofu." Chude alionesha kuwa na hofu. 

"Ya nini tena Chude?" 

"Si juu ya huyu Robinson?" 

"Hilo hata mimi bado ninalo ila naendelea kumchunguza ikiwa ni pamoja kumshirikisha kwenye mambo yangu ya siri ili nione atafanya nini akileta ujuaji atawafuata wenzake." 

Mara Robinson alifika pale akiwa na ile bahasha aliyoagizwa na huku akiwa kaongozana na Melissa. 

"Hii hapa mkuu." Alimkabidhi. 

"Vizuri sasa ishike toa simu yako kisha hizo nyingine chomeni moto hapo pembeni."

"Bosi hapana sihitaji hiyo simu ambayo nilinunuliwa na malaya ambaye alitaka kukuteketeza wewe kama kuchomwa zichomwe zote tu simu nitanunua kwa hela zangu mwenyewe." 

"Robinson kwa sasa umekomaa hebu hii bahasha isiyo na maana kwetu itupe huko porini tunachelewa zetu mjini, na wewe Melissa vipi unaongozana nasi?" 

"Bosi unanijua vizuri mambo yangu nabaki vipi halafu natakiwa kupitia pale maskani kuweka mji sawa." 

"Bila shaka tunaweza kuondoka." Santana aliongea baada ya kuhakikisha ile bahasha imetupwa na Robinson. 

Waliondoka zao na kutoa nafasi kwa Roberto aliyekuwa kajificha kuibuka na kuifuata ile bahasha iliyotupwa. 

"Ina maana wale wadada wameuawa tayari? Na huyu aliyekuwa anaongea na Santana ni nani mbona anaonekana kuwafahamu sana wakina Jackline?" Nitakula sahani moja na Melissa mpaka nijue kisa cha wakina Jackline kuuawa na Santana."

Alijisemesha mwenyewe akiwa anaiendea ile bahasha. Aliichukua na kuifungua baada ya kuifungua alikutana na simu mbili akazitoa na kuzikagua.

"Sasa, ina maana hizi simu ni za nani sasa kati ya wale madada? Najua moja itakuwa ni ya huyu niliyemsikia akiitwa Robinson na nyingine ni ya nani? Ni ya Jackline, ni ya Jasmine au Jessica? Ngoja nitajua tu nikifika tu mjini."

Aliichukua ile bahasha na kuiweka mfukoni kisha akaondoka zake kurudi mjini kwani aliona kuendelea na zoezi la kuwafuatilia wakina Jackline ambao tayari wamekufa ni sawa na kazi bure hivyo ambacho alikiona ni kurudi zake mjini ili ajue cha kufanya japo tayari mtu wa kwanza kuanza naye alikuwa ni Melissa.

Msafara wa Santana ukiwa ndani ya msitu ule wa Amazon mara waliiona gari mbele yao ikiwa katikati ya barabara.

"Hee hii gari si ya kwangu? Mbona iko hapa?" Santana aliuliza alipoiona.

"Ni yenyewe mkuu."

"Sasa ikoje si niliambiwa kwenye simu kuwa gari imepata ajali mbaya na dogo Hassan kafariki? Hebu simamisha gari mara moja."

Gari ilisimamishwa na kisha wote walishuka na kuiendea ile gari kuangalia kulikoni.

"Bosi hakuna mtu ndani ya gari lakini funguo iko mahala pake."

Tom alitoa taarifa baada ya kuichungulia kupitia kwenye kioo cha mlango na baada ya kuufungua mlango ulifunguka.

"Hebu jaribu kuiwasha tuone." Santana aliagiza.

Tom aliingia na kuiwasha lakini haikuwaka, akajaribu tena lakini haikuitikia akashuka.

"Bosi inawezekana imeharibiwa makusudi hii na aliyeiacha hapa."

"Okay inawezekana lakini Hassan yuko wapi?" Santana aliuliza akiwa kauma meno.

"Bado tuna kazi ya kufanya kijana wangu nilijua kufa kwa wale mabinti tungepumzika kumbe tulikuwa tunajidanganya muziki ndiyo kwanza umeanza."

Mzee Bruno Gautier aliongea kwa sauti ya huruma sana nafikiri hii imekuja baada ya mke wake kutoonekana mpaka sasa. 

"Ingieni garini haraka hiyo iacheni hapo hapo kuna kitu tunatakiwa kufanya muda huu."

Aliongea Santana huku akiwa anakuna kichwa kwa nguvu simu ikiwa mkononi akitafuta namba fulani ambayo alipoipata aliipiga.

"Shenzi kabisa namba ya Hassan haipatikani kwa sasa ninahisi yule kijana aliyejifanya msamaria mwema ni kichomi kingine kwetu, tunaelekea kwa Melissa muda huu."

Aliingia garini na kuubamiza mlango kwa nguvu akafunga mkanda na kuruhusu gari iondoke.

Safari ilianza kuelekea North Angle kwa Melissa ambako walihisi kuna chanzo cha tatizo kwa kuwa walimtuma kufuata simu ya Jackline nyumbani kwa Melissa.

Baada ya mwendo mrefu safari yao ilitia nanga getini kwa Melissa ambako Santana alishuka haraka huku kundi lote likimfuata nyuma na alipoufikia mlango wa geti alikuta ukiwa haujafungwa kwa komeo ukiwa umeegeshwa tu na hapo akajua kuna tatizo. Akageuka nyuma kuwapa ishara ya kukamata silaha zao tayari kwa shambulizi.

"Tom na Chude ingieni ndani kwa tahadhari ninyi wengine izungukeni nyumba mimi nitabaki hapa peke yangu." Santana alitoa maelekezo kwa watu wake.

Pasipo kupoteza muda walielekea kwenye maeneo waliyopangiwa na Santana huku Tom na Chude wakiingia ndani kwa tahadhari kubwa na baada ya kukitingisha kitasa kilifunguka bila ubishi kitendo kile kiliwafanya wakina Tom kutazamana kwanza maana ndani inaelekea kuna mtu. Hivyo waliingia kwa kupokezana na baada ya kuingia pale sebuleni walikutana na hali waliyoiacha lakini ile simu hawakuiona. Tom baada ya kuchungulia kwenye korido la kuingia chumbani aliweza kuona mtu kalala chini.

"Chude kuna mwili wa mtu kule koridoni." Tom alimnong'oneza Chude sikioni na Chude naye baada ya kuangalia alikooneshwa naye aliweza kuona na ndipo walipomfuata baada ya kumtambua ni mwenzao Hassan.

"Mungu wangu Hassan kapoteza maisha?"

Tom aliuliza huku akichuchumaa kumkagua Hassan. Na Chude hakutaka kupoteza muda alitoka nje kutoa taarifa.

"Bosi Hassan yuko ndani ya nyumba."

"Vipi hali yake?" Aliuliza Santana.

"Kapoteza maisha kitambo kwani tayari mwili umeanza kutoa harufu."

"Buuuuu shit!!!!!!!!!! Ni kenge gani aliyepita kwenye njia yangu?" Santana alijiuliza swali kwa sauti.

"Mimi nina mashaka na kule ambako walifikia kwani walisema kuna kijana mmoja alitaka kuwaibia hela ambazo walizipora kwenye boti lakini walimdhibiti na kumpa kichapo na ndipo alipofunguka matatizo ya mama ambapo wakina Jackline waliamua kusaidia huyo kijana hivyo asije kuwa ni huyo." Melissa alipata mashaka kuwa inawezekana mfanya yote hayo atakuwa ni Roberto.

" Huyo kijana unamfahamu ni nani na anaishi wapi au huyo mama yake kalazwa wapi? " Santana aliunganisha maswali mfululizo kwa Melissa.

" Hapana simfahamu kwa hawakuweza kumtaja wala sehemu ambayo anaishi huyo kijana." Melissa alifafanua.

"Melissa unaongea nini sasa wakati huna uhakika na kauli zako?" Santana alimfokea Melissa akiwa kamkaribia usoni kabisa.

"Nisamehe bosi wangu nilikurupuka tu kwa bahati mbaya." Melissa alijitetea baada ya kuona kuna dalili ya kukutana na shetani mtoa roho.

"Uchukueni mwili wa Hassan na haraka sana kautupeni pembezoni mwa mji kisha rudini hapa haraka hili eneo si salama hata kidogo."

"Sawa bosi."

Waliitikia wakina Robinson na kuuchukua mwili wa mwenzao na kuupakia kwenye gari na kuondoka kutoka nje ya mji na kuwaacha wakina Santana pale ndani na huku Melissa alianza kuchukua vitu vya msingi kwake tayari kwa kuiacha nyumba yake ambayo kwa wakati huo alihisi ni jehanamu ndogo. Wakati Melissa akiwa anajiandaa mzee Bruno alikuwa katulia tu akimuangalia Santana ambaye alikuwa akichezea simu na katika piga piga namba fulani iliweza kuita.

"Santana, Santana hivi unafikiri hii dunia utaigeuza geuza unavyotaka eee?" Roberto aliuliza baada ya kupokea simu ya Santana.

"Wewe ni nani ambaye na jina langu unalifahamu?" Santana aliuliza.

"Ni mapema sana kunijua kwa sasa brother Santana, ila tu muda ukifika utanijua mimi ni nani na wakati huo nitakuwa mbele yako nikiichukua roho yako na usihofu katika hilo kwa sababu wewe ni utakuwa wa mwisho baada ya kushuhudia kifo cha Melissa atakayeanza, akifuata mzee wangu Bruno kisha Chude na Tom huyo boya wako mgeni yeye atauawa na aliyemleta Brazil." Roberto alimtisha Santana kwa maneno ambayo yaliweza kumpa ubaridi.

" Wewe acha kunitisha inawezekana huna taarifa hao kenge wako kwa sasa ni marehemu na muda huu wako kwa sir God wakijibu maswali magumu."

"Ha ha ha ha ha Santana unajidanganya bro lile kundi bado lipo na kama huamini subiri hata baada ya miaka ishirini utaona mwenyewe."

Baada ya kumhakikishia Santana kuwa asifikirie wakina Jackline wamekufa bali wako hai alikata simu na kuizima kabisa.

"Huyu ni nani? Ambaye anatujua wote kwa majina yetu? Na kanihakikishia kuwa wale Pimbi hawajafa wako hai, inawezekana kweli?" Santana aliuliza swali ambalo hakujua atalijibu nani.

"Huyo anajaribu kukutia jamba jamba tu hajui lolote inawezekana ni hawa madogo wa mjini ambao hutumia madhaifu yetu kujipatia mkwanja." Mzee Bruno Gautier alijaribu kumtuliza mkubwa wake wa kazi.

"Sawa mzee ndiyo atufahamu wote kwa majina mpaka huyu Robinson? Hapa kuna tatizo na tunatakiwa kuwa makini kwani bila kufanya hivyo tutajikuta tukifa mmoja baada ya mwingine ikiwa aliweza kummaliza Hassan humu ndani atashindwaje kwa wengine?" Santana alianza kuingiwa na hofu kutokana na ile simu ya Roberto.


****



Ni alfajiri na mapema ndani ya bahari ya Atlantiki kusini wavuvi wakiwa kwenye shughuli zao ndani ya boti ya uvuvi wanafanikiwa kuuona mwili wa mtu majini ukielea.

" Jamani angalieni pale si mtu yule?"

Mmoja wao aliwaonesha wenzake baada ya kuona mwili wa mtu majini.

"Ni kama mwili wa mtu ule." Mwingine alijibu.

"Mustapha ingia haraka majini tumpe msaada huyo mtu." Aliagiza mzee ambaye alionekana ni kama baba yao kwenye ile boti.

"Sawa mzee."

Mustapha alijibu na kuchukua boya akalivaa na kujirusha majini akapiga mbizi mpaka kwenye ule mwili na kuanza kuuvuta. Aliuvuta mpaka karibu na boti kisha akarushiwa kamba ambayo aliitumia kumviringisha na kisha wakaanza kuuvuta ule mwili mpaka juu.

Mzee yule alipiga magoti na kulitegesha sikio kwenye kifua cha yule mtu.

"Hee mapigo ya moyo yanapiga kwa mbali sana hebu tusaidiane kumkandamiza sehemu ya tumbo kumtoa maji."

"Halafu ni kamdada baba katapona kweli?"

Mustapha alimuuliza baba yake.

"Tuombe Mungu anaweza kupona tu."

Wakiwa wameelekeza nguvu zao katika kuminya tumbo la yule mwanamke waliyemuokoa mara wakaona miili mingine miwili ikiwa inaelea majini.

"Baba kuna nini leo angalia miili mingine ile pale." Alionesha kijana mwingine.

Hapo sasa waliona haina haja ya boya tena vijana wawili walijifunga kamba viunoni na kujirusha kwenye maji na kuifuata miili ile ambayo waliifikia na kuanza kuivuta mpaka kwenye boti.

" Halafu wote ni wasichana hawa inaonekana kuna tatizo walikotoka."

Mzee yule aliongea wakati wakiwatoa maji tumboni.

"Inawezekana ndiyo hawa wakimbizi wanaotupwa majini kila kukicha." Aliongeza mtoto wake mwingine.

"Jamani boti ielekee nyumbani ili tukawawaishe hospitali kwa matibabu zaidi."

Mzee alitoa maagizo na hapo hapo boti lilizungushwa kutoka eneo hilo na kurudi tena mpaka Namibia ambako ndiyo makazi yao. Walitia nanga ndani ya bandari ya Namport.


NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post