NITAKUUA MWENYEWE - 45 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 45

sultanuwezotz.blogspot.com 


Baada ya kutia nanga pale Bandarini Namport waliwashusha na kuwapakia kwenye Ambulance ya bandari na kuwakimbiza mpaka hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE. Na walipowasili walipokelewa na vijana wa mapokezi ambao walileta vitanda maalum vya wagonjwa na kuwashusha na kuwapakia juu yake na kuwakimbiza mpaka Emergency Room tayari kwa uchunguzi. Baada ya taratibu zote kufanywa na madaktari wa KMC waliwapeleka moja kwa moja mpaka kwenye chumba cha joto kutokana kugundulika kuwa wagonjwa walikuwa wamepatwa na tatizo la baridi kutokana na kukaa muda mrefu baharini na kingine kilichowashangaza kwenye vipimo ni mabinti hao kukaa majini kwa muda mrefu bila kupoteza maisha wakati si jambo la kawaida kwa binadamu na pia waliendelea kujiuliza nini kiliwakuta. Na ndipo Daktari Mkuu wa kitengo cha Dharura aitwaye Abass Mukesh alipomuomba mzee Jerome Whistle aliyewaleta wagonjwa hao kwa mazungumzo ofisini kwake.

"Ndiyo mzee wangu naitwa Daktari Abass Mukesh ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya Dharura."

"Nashukuru sana daktari, mimi naitwa mzee Jerome Whistle mvuvi na mfanyabiashara wa samaki hapa Namibia."

"Ndiyo mzee Jerome naomba unieleze ilikuwaje mpaka kukutana na hawa wagonjwa?"

"Daktari ilikuwa hivi, mimi na wanangu tukiwa majini kama kawaida yetu tukivua samaki mara tukapata kuona nguo ikielea juu ya maji na baada ya kuangalia vizuri tukagundua ni mtu ndipo nilipomtaka mwanangu Mustapha aingie majini kumpa msaada mtu huyo lakini tukiwa bize na huyu mgonjwa kumpa huduma ya kwanza ndipo tukawaona na hawa wengine wawili na ndipo wanangu tena Mustapha na Victor walipojitosa kuwaokoa na baada ya kuwaokoa na kuwapa huduma ya kwanza ndipo tulipoizungusha boti yetu na kuwakimbiza hapa kwa huduma Daktari."

Mzee Jerome Whistle alitoa ufafanuzi juu ya kile walichokifanya kwa wagonjwa.

" Aisee ni watu wachache sana wenye moyo kama wako mzee Jerome kwani angekuwa mwingine wala asingejaribu kupoteza muda wake kuwaokoa watu asiowajua na kuacha shughuli zake ila kwako imekuwa tofauti sana nikupe hongera kwa hilo mzee wangu."

"Nashukuru Daktari."

"Vipi mliweza kupata vielelezo vyovyote vinavyowatambulisha hao mabinti?"

Daktari alimuuliza mzee Jerome Whistle.

"Hapana Daktari hatukuweza kupata chochote kile nadhani iwapo watazinduka watatueleza wenyewe kipi kiliwapata huko walikotoka."

"Okay sawa mzee, itabidi iwe hivyo lakini nitakachokuomba mzee ni kwenda kutoa taarifa polisi."

Mzee Jerome alimuangalia kwa muda daktari kama alikuwa akiyachambua maneno yake na ndipo alipokuja na majibu yake.

"Kwa hilo ningeomba libaki siri kati yetu na wewe daktari kwa sababu hatujui kilichowatokea huku tuwasubiri walejewe na fahamu zao watueleze kilichowapata kisha tutajua iwapo tukaripoti au la."

"Basi sawa mzee wangu mimi nakusikiliza wewe, nikushukuru kwa kukubali kupoteza muda wako kuja kuzungumza nami."

"Daktari usijali tuko pamoja katika hili nitakuwa bega kwa bega nawe mpaka tamati."

"Bila shaka mzee Jerome."

Baada ya kuhitimisha mazungumzo yao waliagana na kisha wakatoka ofisini mzee Jerome akawafuata vijana wake huku daktari Abass Mukesh akielekea kwenye kile chumba walichohifadhiwa wakina Jackline.

"Vijana wangu tuondoke nimeshaongea na daktari tayari tutarudi kesho kuwajulia hali wagonjwa wetu kama mjuavyo hawa ni wetu kuanzia sasa."

"Baba kwani daktari kasemaje kuwahusu?"

Victor alimuuliza baba yake juu ya kile alichokiongea daktari.

"Kasema kuwa tuwaache waendelee kuwafanyia uchunguzi wa kina lakini wakianza na kuwapandishia joto kwanza na hivyo kasema mpaka kesho majibu yatakuwa yamepatikana."

Mzee Jerome alifafanua kwa watoto wake, kisha waliondoka eneo hilo la hospitali kurudi kwao.

" Wale mabinti imekuwaje mpaka wakutwe na janga lile la kutupwa baharini? Ni wakina nani hawa?"

Mzee Jerome alikuwa akijiwazia wakiwa ndani ya gari la jumuiya wenyewe wakiyaita townbus' huku Tanzania tukiyaita daladala na wenzetu kule Kenya wakiyaita Matatu.

" Wanangu hebu tushukie hapa hapa Independence Tower' "

" Baba si umetuambia tunaelekea nyumbani mbona umepingana na uamuzi wako mwenyewe?"

Mustapha alimuuliza baba yake ambaye alionekana kupata wazo jipya na hivyo kuamua kushuka kabla ya kufika nyumbani.

"Nyumbani tunakwenda ila nimeona tupitie hapo kwenye duka la Kahawa tuweze kuamsha matumbo si mnajua hatukuweza kupata chochote toka jana usiku."

"Ni kweli kabisa baba maana si kwa baridi hii ninayoisikia tumboni." Victor alionekana kuifurahia ofa ya baba yao aliyowaambia.

"Ndiyo hivyo wanangu na si kingine chochote kile."

"Tumekuelewa baba, tuwahi tusije ambulia vikombe tupu." Victor aliona awachekeshe wenzake.

"Muuza kahawa uko wapi? Tupatie vikombe vitatu tafadhali." Mzee Jerome Whistle aliagiza.

"Sawa mzee naleta."

Muuza kahawa alijibu huku akifungua kabati la vyombo.

"Kaka tufanyie haraka tuna majukumu mengine ya kifamilia bwana."

Victor alimharakisha muuza kahawa pale ndani.

Roberto akiwa nyumbani kwao maeneo ya Rio Branco anazitoa simu zile tatu yaani ile ya Jackline aliyoichukua kule nyumbani kwa Melissa na zile mbili alizoziokota kule porini Amazon baada ya kutupwa na Santana. Aliziweka mezani zote na kuziwasha zote na kama bahati vile zote ziliwaka ila shida ikawa kwenye ile aliyoichukua nyumbani kwa Melissa kwani ilikuwa na nywila akaona isiwe taabu kwake akaiweka kando na kuzirudia zile mbili akaanza na ile ambayo ilikuwa na picha ya Jackline akiwa kakumbatiana na Robinson.

"Nimepata jibu hapa hawa walikuwa ni wapenzi kabla ya kuchenganaaa Okey!!!!"

Aliifungua upande wa 'All calls' na kuanza kuangalia simu hiyo iliwahi kufanya mawasiliano na watu gani ndipo alipoona baadhi ya majina kama My father in-law, my young sister, na jingine lilikuwa ni la Simbozya ndiyo majina ambayo yalionekana kufanya mawasiliano na simu ya Jackline. Akaiweka kando kisha akachukua ile nyingine ambayo nayo ilikuwa na picha ile ile kama wallpaper' ya simu kitu ambacho kilimthibitishia moja kwa moja Jackline na Robinson walikuwa wapenzi.

"Mhh hayanihusu hayo mimi nifanye kazi yangu niliyoikusudia."

Alijiwazia mwenyewe baada ya kuona ile picha. Kisha akaifungua upande wa miito na kuangalia namba zilizofanya mawasiliano na simu hiyo ndipo alipokutana na majina mawili tu ambayo ni Baba na Shamimu na alipojaribu kuangalia namba ile iliyoandikwa baba akaona ni ile ile ambayo iko kwenye simu ya awali iliyoandikwa My father in-law na ile nyingine iliyoandikwa Shamimu akaona ni ile ile iliyoandikwa my young sister na hapo ndipo akapata sehemu ya kuanzia na kuona hakuna haja ya kuifuatilia ile nyingine iliyoandikwa Simbozya, akazichukua na kuziweka chaji zote kisha akatoka na kwenda kwenye kiduka kilicho karibu na nyumba yao kwa ajili ya kununua muda wa maongezi.

"Samahani jirani naomba muda wa maongezi wa shilingi elfu thelathini."

"Jirani wa hela yote hiyo unataka kuwasiliana na nani au unataka kumtumia mtu nini jiraniii?" Alitaniwa na dada yule muuza duka.

"Acha utani basi mtu wangu nifanyie hivyo basi nina haraka kidogo."

"Mmhh okay bwana naona tu siku hizi unazidi kuotesha tu kibanda cha tumbo."

Yule dada aliongea hayo akimkabidhi Roberto vocha zake. Baada ya kumkabidhi hela yake aliondoka zake kurudi nyumbani kukamilisha kile ambacho alidhamiria kukifanya. Aliingia na kuichukua ile simu ambayo alijua ni ya Jackline na kuiingizia muda wa maongezi kisha akaibonyeza namba ya mdogo wa Jackline ambayo ni ya Shamimu na kuipiga, kama bahati vile iliita.

"Jamani dada yangu Jackline ndiyo nini kupotea hivyo hata meseji kwa mdogo wako kweli? Au kwa sababu wazazi wangu hawapo ndiyo umeamua kunitenga kaka kaka? Sawa tu dada yangu ila mimi bado nitaendelea kuwa mdogo wako tu na elewa kwa sasa si mwanafunzi tena ni mhitimu tayari."

Roberto alibakia kuwa msikilizaji tu baada mpigiwa kugeuka kuwa msemaji mkuu badala ya kusikia kile kilichopangwa kuzungumzwa na mpigaji.

Hapo Roberto alibaini kitu kutoka kwa mdogo wa Jackline hivyo akaona kuwa akisema amjulishe kuwa dada yake alishafariki itakuwa nongwa kubwa hivyo aliamua kukata simu. Akaona ampigie simu mtu wa pili ambaye ni baba mkwe wa Jackline ili huyo ndiyo ampe taarifa.

"Waooo mwanangu Jackline, eeehh hujambo mwanangu? Mnaendeleaje huko ugenini na mmefikia wapi? Huku mwanangu mambo ni mazuri sana kwani yule ibilisi tayari yuko ndani akisubiri tu kukabiliana na hukumu yake pindi mkifika."

Roberto alishusha pumzi ndefu kwanza baada ya kuyasikia maelezo hayo ya mzee huyo ambaye naye hakuwa tofauti sana na mdogo wa Jackline ndipo akaona tu ajitose kufikisha taarifa kamili.

" Mzee kwanza shikamoo  !!!! "

Alianza kwa kumsalimu ili kuvuta usikivu kutoka kwa mzee Kaaya.

"Hee ni nani wewe tena ambaye umetumia simu ya mkwe wangu? Au ni Robinson mwanangu?"

"Hapana mzee mimi si huyo mwanao wala si yeyote kwa Jackline bali ni msamaria mwema tu niliokota simu mbili ya mwanao Robinson pamoja na hii ya mkwe wako."

"Unasemaje wewe kijana? Umeziokota kivipi? Mbona unanipa presha?"

"Hapana mzee punguza presha niweze kukufikishia ujumbe niliopanga kukupa mzee wangu."

"Haya nakusikiliza nijuze kulikoni maana tayari jasho la pua linanitoka."

"Ni hivi mzee wangu, mimi naitwa Roberto naishi Brazil nikijuana na Jackline pamoja na rafiki zake wawili Jasmine na Jessica lakini ni kama vile Mungu alinikutanisha nao ili niwe barua yao kwenu."

"Kivipi hapo Roberto bado unaniweka gizani?"

"Baada ya siku kadhaa kupita na kuachana nao nilipata taarifa zao kuwa wameuawa na mtu ambaye ni hatari sana duniani akishilikiana na mwanao Robinson."

"Weee, wewe, weeeeeeee kijana kama ulipanga kuniletea habari za kipuuzi kama hizo jua umenoa mimi si wa aina hiyo na usitegemeee kupata chochote kwangu mimi ni mlala hoi tu kwa hiyo kama umewateka wewe waachie tu ndugu yangu."

"Mzee si..."  Kabla hajamalizia neno lake Roberto alisikia simu ikikatwa na alipojaribu kuipiga tena ilikuwa imezimwa kabisa simu ya mzee huyo.

"Duuu ishakuwa tabu hapatikani tena hewani, nifanye nini sasa Roberto miye ila si mbaya taarifa ameipata kuikubali au kuikataa ni juu yake."

Roberto alijisemesha mwenyewe baada ya kukatiwa simu na mzee Kaaya na mara baada ya kuipiga tena haikupatikana tena.


****


"Dada kapatwa na nini mbona kapiga simu halafu haongei kitu na badala yake amekata simu au ndiyo kusema kachukizwa na maneno yangu?"

Shamimu alikuwa kajishika mashavu akifikiria kitendo cha kukatiwa simu na mtu aliyejua ni dada yake Jackline.

"Shamimu mwanangu mbona umejikunja hivyo hapo kulikoni?" Mama Robinson alimuuliza baada ya kumuona akiwa kajikunja pale nje ya nyumba.

"Hamna kitu mama." Alijibu huku akijifuta machozi na pembe ya kitenge chake.

"Si kweli hata kidogo mwanangu huwezi sema hakuna kitu ilhali unatokwa na machozi?"

Mama Robinson alimuuliza tena huku akikaa karibu yake kutaka kujua kinachomliza.

"Mama hakuna kitu ni dada Jackline tu huyu."

"Kafanya nini tena wakati unajua bado hajarudi toka safari yake?"

"Amenipigia muda si mrefu mama."

"Acha uongo mwanangu Jackline huyu huyu kakupigia simu? Hajanisalimu?"

"Kukusalimu tena mama wakati nilipopokea tu nikamtolea dukuduku langu lote hee si ikawa tabu mama akanikatia na nimejaribu kumpigia tena hapatikani."

"Jamani pole sana mwanangu ndiyo kinakuliza hicho, usilie bwana si unajua kwa sasa dada yako ana msongo wa mawazo?"

"Najua mama."

"Ehhh basi ndiyo maana kakukatia simu akifikiria kuwa hujali anachokifanya na kuangalia upande wako, ila najua hajakuchukia atakupigia tu wakati mwingine tumpe muda."

"Sawa mama." Shamimu alijibu na kuinuka kuelekea ndani akimuacha mama Robinson akiwa kaketi.

"HABARI ILIYOTUFIKIA HIVI PUNDE...

Watu watatu ambao jinsi yao ni kike wameokolewa na Wavuvi wa Kinamibia kutoka ndani ya bahari ya Atlantiki. Kwa sasa wanapatiwa matibabu ndani ya Hospitali ya KING'S MEDICARE CENTRE.

TUNAENDELEA KUIFUATILIA HABARI HII KWA UNDANI ZAIDI."

Habari hiyo kutoka Kituo kimoja cha Televisheni aliyokuwa akiiangalia iliweza kumshtua mzee Kaaya ambaye muda mfupi uliopita alipokea taarifa kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kwa jina la Roberto.

" Baba taarifa hiyo imetokea wapi?" Shamimu aliuliza baada ya kuiona ikiishia wakati yeye akiingia ndani kutoka nje.

"Sijui imetokea wapi hiyo mwanangu hawajatoa ufafanuzi." 

"Hivi kwanini siku hizi watu wanauawa sana baharini?" Shamimu aliuliza. 

"Mwanangu bara letu la Afrika lina matatizo mengi sana ambayo wengi yamewashinda na kuamua kutorokea nje ya bara ili kujaribu bahati yao lakini shida inayokuja ni njia ambazo zinatumika na wao si rasmi mwanangu." Mzee Kaaya alifafanua kwa mwanaye.

" Ni kweli kabisa baba, kwa matatizo yanayotukumba watu wenye ngozi nyeusi unaweza jikuta ukitimkia huko na hata tukisema wafuate njia halali hawawezi kufanikiwa haraka."

"Mwanangu mbona umeniacha mwenyewe nje?" Mama Robinson alimuuliza Shamimu.


NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post