NITAKUUA MWENYEWE - 46 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 46

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Niliamua kuingia ndani baada ya kuona hapo nje kuna mbu mama." Shamimu alimjibu mama yake. 

"Sawa mwanangu hata mimi kimenikimbiza hicho hicho na sijajua nini kimepelekea mbu kuwa wengi mwaka huu?" Mama Robinson alirusha swali hewani ili yeyote alijibu. 

"Hakuna chochote mke wangu zaidi ya madimbwi ya maji huko nyuma pamoja na majani yaliyokuwa sana ndani ya mtaa wetu." Mzee Kaaya alimjibu mke wake. 

"Tukiamka salama kesho nitaifanya kazi hiyo ya kufukia mashimo ya maji pamoja na kupalilia nyasi zote kuzunguka nyumba yetu." Shamimu aliwaahidi walezi wake kuifanya kazi hiyo. 

"Vizuri mwanangu na mimi nitakuunga mkono."

Mama Robinson alimuahidi kuungana naye kufanya usafi huo ambao utapelekea kuondoa mazalia ya mbu. 

"Sawa mama." Shamimu alijibu huku akiingia jikoni kufanya maandalizi ya chakula cha usiku. 

"Mume wangu leo jambo la ajabu limemtokea Shamimu ambalo sikulitegemea kabisa." 

"Jambo gani hilo mke wangu." 

"Si Jackline alimpigia simu lakini cha ajabu hakuongea chochote zaidi ya kumsikiliza tu mdogo wake na kisha kuikata bila kuongea chochote." Maneno yale ya mke wake yalimshtua tena mzee Kaaya na moja kwa moja akajua huyo wala Jackline bali ni yule yule aliyempigia yeye hata hivyo hakutaka kumshirikisha mke wake kile alichokisikia kutoka kwa Roberto kwa kuhofia kuzalisha tatizo kutokana na mke wake kumpenda sana mtoto wake Robinson. 

"Inawezekana alikuwa kwenye eneo ambalo mtandao uko chini sana ndiyo maana aliona akate simu mpaka apate sehemu nzuri." Mzee Kaaya alimjibu mke wake. 

"Inawezekana mume ikawa tatizo likawa ni hilo sasa mwenye dada alipofanyiwa tendo hilo siyo kumwaga machozi kule." 

"Utamuelekeza hivyo ajue asifikiri kila eneo lina mtandao mzuri kwa mawasiliano." 

"Sawa mume wangu, basi ngoja tufanye maandalizi ya chakula maana muda nao umekimbia sana." 

Alijibu mume wake na kuelekea jikoni kusaidiana na Shamimu kuandaa chakula. Na baada ya chakula kila mmoja alielekea chumbani kwake kutoa faida kwa mbu. 

Kulipokucha mzee Kaaya aliona aende Internet Cafe akajaribu kutafuta mawasiliano ya mtoto wake Robinson ili aweze kujua kulikoni mpaka ahusike na kifo cha mwanamke ambaye alimpenda kutoka moyoni pasipo kuangalia maisha yao yalivyo.

"Mtoto huyu kakumbwa na mdudu gani vile mbona sikumlea hivyo na kwa Robinson ninayemfahamu hakuwahi kuua hata panya iweje aue mtu tena mpenzi wake? Nitaiweka wapi sura yangu mimi Kaaya mwenyekiti niliye mstari wa mbele kuipigania familia ya Jackline iweze kupata haki zake sasa kimetokea kidudu mtu ndani ya nyumba yangu mwenyewe daa eee Mungu wangu nipe nguvu yasiwe ya kweli haya."

Alikuwa akiongea peke njiani tena kwa vitendo vya mkono akiwa anaelekea kupata huduma.

" Baba mbona unaongea peke yako njiani?"

Shamimu alimuuliza mzee Kaaya baada ya kumuona akiwa bize anaongea peke wakati yeye akitoka kununua vitafunwa.

" Shamimu mwanangu umetoka wapi muda huu?"

Badala ya kujibu swali aliloulizwa alimtupia naye swali.

"Niliwahi kununua vitafunwa kule kwa mama Mlokozi si unajua kuwa ndiye fundi wa kupika vitumbua unavyovipendaga baba?"

Shamimu alimjibu huku akimkazia macho usoni mzee huyo ambaye alionekana kuwa na mawazo sana. Na baada ya kuona hakuna anachoongea zaidi ya kuchezesha vidole vya mkono kwa kuvipiga piga usawa wa mfuko wa suruali.

" Baaba umenisikia lakini nilichosema?" Shamimu alimtupia swali jingine.

"Mwanangu nimekusikia sasa wewe wahi nyumbani narudi muda si mrefu kuna sehemu nafika mara moja."

"Sawa baba." Shamimu alikubaliana na mzee Kaaya na kuachana naye.

Mzee Kaaya alifika mpaka Gomba Internet Cafe na kukutana na chifu mwenyewe wa Cafe hiyo bwana Gombanila na kumueleza dhumuni lake la kufika hapo na baada ya kusikilizwa sana mzee Kaaya kiongozi huyo wa Cafe hiyo aliingia mtandaoni na kuanza kulifanyia kazi ombi la Mzee Kaaya kumtafutia taarifa zinazomhusu kijana wake Robinson.

Gombanila alitumia zaidi ya dakika kumi tano kuweza kutafuta taarifa hizo lakini hakuweza kuzipata na ndipo mzee Kaaya akatoa simu yake na kumtajia namba ya mtoto wake Robinson na kisha ikatafuta kupitia application maalum ya mawasiliano ambayo gharama zake kwa simu za nje ya nchi si kubwa sana ukilinganisha na kwa njia ya kawaida kisha akaipiga namba ile na kama bahati vile simu iliita.

"Mzee anapatikana jiandae kuongea naye, kaa kwenye hicho kiti kisha vaa hizo headphones tayari kwa kuongea naye akipokea."

Gombanila alimwambia mzee Kaaya wakati akiendelea kufanya koneksheni ya mawasiliano.

Mzee baada ya kuvaa zile headphones system ilikubali na simu kupokelewa upande wa pili.

" Haloo, haloo mwanangu  !!! " Mzee Kaaya aliita.

" Naam mzee kwa bahati mbaya hii simu iko na yule yule aliyekupa taarifa za mwanao jana ambazo hukutaka kuzipokea kabisa na ndiyo maana ulinikatia simu."

"Ni wewe Roberto au nani?"

"Ndiye mwenyewe mzee labda niombe kukusikiliza kwa lile unalotaka kuniambia."

"Sasa kijana wangu Roberto imekuwaje ukawa na simu zote mbili? Ya Robinson pamoja na ya Jackline huoni kama unanipa mashaka?"

"Huna haja ya kuonesha mashaka kwangu mzee naomba ufungue masikio yako vizuri na unisikilize kile ninachokwenda kukuambia leo na kama hutanielewa basi usinitafute tena, mwanao Robinson anahusika na mauaji ya Jackline na wenzake wawili akishirikiana na mtu mmoja aitwaye Santana na ndiyo maana baada ya kuhakikisha zoezi lao la kuwaua limekamilika na kuwatupa baharini waliamua kuzitupa na simu hizi nje kidogo na Ngome yao na kwa kuwa sikuwa mbali na eneo lile baada ya wao kuondoka tu nilizifuata na kuziokota hizi simu na kwa taarifa yako nina mbili za Jackline na moja ya Robinson na pia naomba nikupe tu taarifa nzuri ambayo ni chungu kwako mzee, mimi ndiye ambaye nimeahidi kumkamata mwanao na si kumkamata tu bali na kumuua kwa mikono yangu miwili tena kifo kitakuwa kile kile alichofanya kwa Jackline."

"Kijana huko unakwenda mbali sana mimi nadhani unisaidie kupata taarifa ambazo zitanifanya kupata ushahidi wa mwanangu kuhusika na mauaji."

Mzee Kaaya alianza kushuka kidogo kidogo baada ya kukuta taarifa ni ile ile haibadiliki kutoka kwa Roberto.

"Mzee nakata simu na kisha nakutumia namba ya mtu ambaye anafanya kazi na mwanao."

Roberto alikata simu kisha akaitafuta namba ya Santana na kuituma kwa mzee Kaaya na baada ya kuiona Gomba aliingiza kwenye mfumo na kuipiga namba hiyo.

"Haloo naongea na nani?" Mzee Kaaya alianza kwa kuuliza baada ya simu kupokelewa upande wa pili.

"Wewe umempigia nani?" Santana aliuliza.

"Samahani sana kijana wangu mimi ni ndugu yake Robinson nataka kumpa tahadhari kutokana na kuuawa kwa Jackline kwani kuna mtu yuko kati yenu anawazunguka hivyo kama hutojali naomba niongee na mlengwa." Mzee Kaaya alifanikiwa kuutengeneza uongo.

"Unaishi nchi gani?" Santana alimuuliza mzee Kaaya.

"Mimi naishi Afrika ndani ya kisiwa cha Zanzibar." Mzee Kaaya aliendelea kudanganya.

"Okay nimekuelewa ongea na mtu wako huyu hapa."

Santana ilibidi ampe simu Robinson ili aongee na mtu huyo ambaye hakuwa kamfahamu na bila shaka iwapo angemfahamu wala asingekuwa tayari kumuunganisha na Robinson.

"Ndiyo Robinson hapa naongea, nani mwenzangu?" Robinson alianza kwa kujitambulisha na kuuliza anaongea na nani.

"Ooohhh vizuri sana unahaja ya kutaka kujua unaongea na nani mpaka hapa Robinson?" Mzee Kaaya alimuuliza.

"Ina maa.. ina maana naongea na baba mzee Kaaya?" Robinson alipata kigugumizi baada ya kuitambua sauti ya baba yake.

"Vizuri kama umenifahamu mwanangu, eeh naomba kujua mnaendeleaje huko?" Mzee Kaaya alimuuliza swali la mtego.

"Kabla ya yote mzee ningependa kujua namba hii wewe umeipataje tena ukiwa Tanzania?" Robinson alishachanganyikiwa tayari.

"Nitakujibu kwanza jibu swali langu." Mzee Kaaya alimrudisha nyuma.

"Huku sisi tunaendelea vizuri baba na bila shaka muda si mrefu tutarejea nyumbani."

"Mkwe wangu yuko hapo niongee naye?"

"Ame... ametoka kidogo akirudi nitampa salamu zako."

"Mbona ni kama una mashaka hivi mwanangu? Eeh simu yako iko wapi mbona haipatikani hewani?" Mzee Kaaya alimuamua kumtega mtoto wake.

"Simu yangu baba niliibiwa siku moja nikiwa mjini."

"Okay pole sana mwanangu, lakini mbona namba yako iko na mtu ambaye ana taarifa zako zote na inasemekana simu yako na ya Jackline ulizitupa porini ukiwa na huyu mwenye hii simu?"

Mzee Kaaya aliona ampige swali litakalomshtua kidogo.

Hivyo kama alifanikiwa kwa mpango huo kwani baada ya kulisikia tu hilo swali hakuweza kulitafakari zaidi kwani alikata simu.

" Kwanini amenikatia simu huyu Robinson."

Mzee Kaaya alijiuliza swali hili akiwa anazivua zile headphones.

"Niambie mzee anasemaje mwanao mbona ni kama uliduwaa kwa muda hivi kabla ya kutoa headphones." Gombanila alimuuliza mzee Kaaya.

"Kijana wangu naomba uniambie ni kiasi gani natakiwa kulipa haya mengine tuachane nayo nitayakabili mwenyewe."

Mzee Kaaya alimjibu kijana huyo mwenye internet Cafe baada ya kuona anatafuta ufukunyuku usiomhusu.

"Utalipia shilingi elfu tano pekee mzee wangu."

"Simu za nje hazifai hata kidogo gharama zake ni kubwa sana."

"Na hapo ushukuru nimeitumia system rafiki tofauti na hapo ungejikuta ukitoa zaidi ya shilingi elfu kumi na tano kulingana na muda ulioutumia." Gombanila alimfafanulia mzee Kaaya.

Basi mzee Kaaya aliingiza mkono mfukoni na kutoa kiasi hicho cha fedha na kumkabidhi Gombanila na kisha alitoka zake na kurejea nyumbani kwake akiwa na msululu wa maswali kichwani mwake huku akijiuliza mtoto wake amekumbwa na nini huko Brazil mpaka kufikia hatua ya kujiunga na makundi ya kihalifu.


****


Mzee Jerome na wanaye walijihimu mapema kurejea hospitalini pale KING'S MEDICARE CENTRE kuwahi kuwajulia wagonjwa wao waliowapeleka pale.

Waliwasili na moja kwa moja wakaenda kukutana na daktari bingwa Mr Abbas Mukesh ofisini kwake ili wajue maendeleo yao.

"Ooohhh mzee Jerome Whistle karibu sana naona umeongozana na jeshi lako la Ukombozi."

"Asante daktari wangu ni kweli nimeongozana nao si unajua tena mimi ni Ikulu na wao ndiyo walinzi wa hii Ikulu."

"Aisee vizuri sana mzee wangu, turudi kwenye maendeleo ya wagonjwa wetu toka mlipowaleta ile jana."

"Sawa sawa mtaalam wanaendeleaje kwa sasa?"

"Kiukweli hali yao si nzuri au mbaya sababu mpaka sasa hawajaamka ila nina matumaini makubwa ya wao kuzinduka. Ila kuna kitu ambacho nina mashaka nacho mzee."

"Kipi hicho daktari wangu?"

"Ni kuvuja kwa taarifa zao."

"Kuvuja?"

"Ndiyo mzee jana baada ya ninyi kuondoka nilifungua laptop yangu na kuangalia duniani kuna nini ndipo nikakutana na taarifa ya kuokolewa kwao ikiambatana na picha zao japo hazikuonesha sura zao."

Daktari Abbas alimwelezea mzee Jerome huku akiifungua PC yake ili awaoneshe taarifa ile ambayo ililipotiwa na blog maarufu ya habari nchini humo Namibia ya fantasticnewz.

" Walizipata wapi hizi taarifa hawa jamaa?"

" Nina mashaka na pale bandarini maana hata mazingira haya ukiyaangalia vizuri ni ya pale."

"Hebu tuone, yes daktari hapo ni bandarini kabisa daa sijui itakuwaje?"

"Mimi nina wazo ambalo litakuwa ni msaada kwako na wagonjwa wako."

"Lipi hilo daktari?"

"Ni kuwatoa hapa kwa siri kubwa na kuwapeleka ndani ya jiji la Windhoek pale kuna hospitali ya rafiki yangu inayojulikana kwa jina la Makambi Hospital pale kuna VIP room ambazo ziko chini nina uhakika watapata huduma nzuri mpaka kupona kwao."

"Sasa daktari kama ujuavyo kule Windhoek ni mbali kutoka hapa itakuwaje?" Mzee Jerome alimuuliza daktari.

"Kuhusu hilo ondoa shaka ile hospitali ina helicopter ya huduma ya kwanza ambayo huitumia kwenye kambi mbalimbali za utalii nchini hivyo nitamjulisha na kupelekea wao kutuma ndege hiyo ambapo mida ya saa tano usiku tutawasafirisha kupitia mlango wa dharura ambao uko kwenye kitanda alicholala yule binti mwenye kidonda mguuni."

" Nitashukuru sana daktari wangu kwani baada ya blog hii kusambaza habari hii bila shaka itakuwa imesambaa sana duniani na kupelekea wabaya wao kuanza kuwafuatilia tena ila kwa plan hiyo wataambulia manyoya hapa."

"Na ndiyo maana nilipata wazo hili kwani huu mtandao una fans wengi sana duniani na nikajua moja kwa moja lazima wabaya wao wataanza kuwafuatilia."

"Nikushukuru sana daktari kwa kufikiria hilo na niko tayari kuelekea huko nikiwa na vijana wangu hawa na kama hutojali tunaomba tukawaone kisha turudi nyumbani kujiandaa na safari."

"Bila shaka mzee Jerome."

Walitoka na kuelekea kwenye kile chumba walicholazwa wakina Jackline.


*****


"Hivi Robinson unaweza kunieleza baba yako kazipata wapi taarifa hizi na si hizo tu na pia namba yangu kaitoa wapi?"

Santana alimuuliza swali Robinson mara baada ya mzee Kaaya kuwapigia simu.

"Yaani hata mimi nina mashaka na hilo japo wasiwasi wangu ni yule aliyekupigia simu kupitia simu ya marehemu Hassan."

"Yes hapo naanza kupata wasiwasi na huyo mtu ni nani na anaishi wapi?" 

Na hapo hapo akapata wazo la kumpigia simu mmoja wa vijana wake kule kambini na kutaka aende pale nje kwenye vile vichaka na kuzitafuta zile simu ambazo zilikuwa kwenye kimfuko maalum. Kisha alitulia kusubiri taarifa ya huyo kijana aliyemtuma.

Na baada ya muda simu iliita na alipoipokea tu ilimfanya atokwe na jasho la ajabu.

"Kasemaje bosi?" Chude aliuliza swali baada ya kumuona bosi wake akiitoa simu sikioni na kujishika kiuno huku akigongagonga mguu chini.

"Wamezitafuta bila mafanikio yoyote hawajaziona."

"Zimekwenda wapi sasa?" Robinson aliuliza. 

"Hilo ndiyo swali la kujiuliza vijana wangu."

Baada ya hapo waliingia garini na kurudi kambini kufanya oparesheni ya kumsaka mtu anayecheza na akili yake.

"Bosi hebu iangalie hii taarifa hapa?" Melissa alimuonesha Santana taarifa fulani hivi ambayo yeye mwenyewe Melissa ilimshtua.

"What???????? Ina maana hawa panya wameokolewa? Nooooo sikubali hata kidogo."

Santana alipiga kelele za maswali baada ya kuona taarifa ya kupatikana kwa wakina Jackline huko Namibia.

"Hivi ninyi mliwatupa kweli au mliwapakia kwenye Meli nyingine?" Santana aliwauliza wakina Robinson.

"Bosi huo ni muujiza huwezi amini kwani sisi tuliwatupa kabisa shahidi ni giza ambalo lilikuwa linatupiga chabo." Chude aliamhakikishia bosi wake.

"Hapa tuache malumbano jamani cha kufanya ni kupanga mkakati wa kuwapata na kuwamaliza kabla hawajapona." Mzee Bruno Gautier aliwauliza vijana wake.

"Hilo neno mzee wangu." Melissa alimuunga mkono mzee Bruno Gautier.

"NAITWA JACKLINE JOACHIM KUANZIA LEO NAKUWA KIVULI CHENU POPOTE MLIPO NIPO NA KAMA MLIJUA TUMEKUFA KULE BAHARINI MSAHAU KABISA TUKO HAI KABISA NA HAPA NAJUA MNAPANGA NAMNA YA KUTUKABILI KARIBUNI SANA."

Ni ujumbe ulioingia kwenye simu ya Santana kupitia mtandao wa Whatsapp na ndipo Santana alipoiangalia ile meseji akaisoma na kisha pale pale akaichunguza ile namba iliyotuma ule ujumbe, cha ajabu akakutana na namba ya Robinson.

" Jamani hebu twendeni kambini kwanza maana kichwa changu kina uma sana angalieni huu ujumbe uliotumwa kupitia namba ambayo tuliitupa pale msituni na ambayo muda mfupi uliopita wamezikosa."

Kila mmoja aliusoma ule ujumbe na kuishia kutoa macho tu wakiwa hawajui wafanye nini kwani tayari mbaya wao wanatembea naye popote walipo.


NDUGU MSOMAJI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


        #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post