NITAKUUA MWENYEWE - 63
sultanuwezotz.blogspot.com
Ilikuwa ni mchana wa saa saba jua likiwaka kwa kuibiaibia huku wingu likiwa limechukua nafasi kubwa na kuifanya hali ya hewa kuwa ya ubaridi sana, kila mtu alionekana akiwa ndani ya nguo nzito ambazo muda wote ni kupambana na baridi kali ya mkoa huu. Lakini cha ajabu ilikuwa ni kwa baadhi ya vijana walioonekana kuifurahia hali hii ya hewa kwani walikuwa vifua wazi wakibebelea mizigo kutoka kwenye jengo moja ambalo ni kama ghala ya kuhifadhia mizigo na bidhaa mbalimbali likiwa nje kidogo ya Uwanjani wa Ndege wa Songwe.
Hii iliwafanya wapita njia kuwashangaa muda wote. Kwenye gari ndogo aina ya Toyota Brevis nyekundu yenye chapa maalum ya usafirishaji abiria kutoka Uwanja wa Ndege kuwapeleka katikati ya mji na nje kidogo ya mji wa Mbeya, pembeni ya dereva huyu mtanashati alitulia mrembo mmoja ambaye kwa muonekano tu alikuwa ni mgeni wa jiji la Mbeya kutokana na kushangaa kila alichokuwa anakiona mbele au pembeni yake na muda mwingi alionekana kuiangalia sana simu yake ambayo masikioni kulikuwa na wireless phones ambazo ukizitazama kwa haraka unaweza kusema ni hereni kumbe la.
"Tutachukua muda gani kutoka hapa mpaka Forest mpya?"
Mrembo huyo alimuuliza dereva ambaye muda mwingi alikuwa akiibia kwa jicho la pembeni kuuangalia uzuri wa abiria wake.
"Samahani umesemaje dada yangu?"
Ilibidi aulize kwa kuwa alipokuwa akiulizwa swali yeye alikuwa safarini kimawazo na kwa inavyoonekana tayari alishapata ugonjwa wa matamanio.
"Nimeuliza hivi, itatuchukua muda gani kufika Forest mpya?" Ilibidi arudie tena swali lake.
"Ni dakika ishirini tu ila lingekuwa ni gari bovu bovu mwenyewe ungeisoma mngechukua hata masaa mawili au zaidi."
Dereva alitamba mbele ya mrembo kwa kuisifia gari yake.
"Ni kilometa ngapi?" Alipigwa swali jingine tena.
"Ni kama kilometa nane mpaka kumi hivi ila sina uhakika sana."
Majibu ya dereva yalimfanya mrembo huyo kutabasamu kidogo bila shaka alibaini kitu.
"Naitwa Mwakapera dereva mashuhuri hapa Songwe Airport nikihudumia abiria wa ndani na nje ya Tanzania nikihakikisha usalama wao kwa asilimia mia moja sijui mwenzangu wanakuitaje?"
"Naitwa Titiana Thompson."
"Aisee jina zuri kama wewe mwenyewe."
"Nashukuru sana."
Alijibu huku akiiangalia simu yake ambayo ilikuwa kwenye tracking system na alipoiangalia vizuri ikamuonesha kuwa ni mita kadhaa mbele anatakiwa kusimama.
"Samahani kaka yangu naomba unishushe hapo mbele kwenye hilo bango kubwa."
"Mbona bado si umesema Forest mpya?"
Dereva alimuuliza baada ya kuona akitaka kushushwa eneo la Maghorofani.
"Ni kweli lakini naomba uniache hapo hapo nadhani unaiona hiyo Corolla nyeupe pale mbele ya lile bango."
"Ndiyo nimeiona."
"Vizuri hapo ndipo usimame tafadhali."
Dereva ilibidi awe mpole kwani hakuwa na la kufanya zaidi ya kutekeleza matakwa ya abiria wake na baada ya kufika pale gari lilisimama kisha akatelemka mrembo Titiana kisha dereva naye akatelemka na kushusha mizigo yake. Baada ya kupokea hela yake alimshukuru na kugeuza gari kurudi alikotoka huku ndani ya ile Corolla alishuka kijana mmoja mweupe na mwembamba mwenye nywele nyingi kiasi zikiwa ndani ya kofia aina ya cap nyekundu na machoni akiwa katupia miwani mikubwa myeusi kwa upande wa miguuni alikuwa na Raba nyeupe ambazo hazikuwa na nembo yoyote ile huku jeans ya rangi ya nyeusi na t-shirt nyeupe ikiwa ndani ya Kikoti cha rangi ya kijivu vikiupamba mwili wake. Walikumbatiana na kisha waliingiza mabegi kwenye gari hiyo na wao wakaingia zao na safari ikaanza.
"Nipe habari mpenzi?"
"Freshi tu baby niliingia hapa usiku wa saa tisa mvua ilikuwa ikipiga balaa baridi usiseme, nchi hii si ya kawaida nishukuru Mungu dereva huyu alinipa kampani ya nguvu sana kwani alinifikisha MBEYA SMILE HOTEL iliyo Forest mpya nilijitupa bila kula kitu chenye chochote kile mpaka asubuhi nikapata chochote kitu ndiyo kuwa sawa."
Roberto ambaye alitangulia kwa masaa kadhaa mbele ya mpenzi wake Titiana Thompson alikuwa akimpa mchapo wa safari yake ilivyokuwa.
" Pole sana mpenzi wangu lakini hali hii inakaribiana na ya kwetu Brazil sema hapa ni kama imezidi kidogo."
"Hapana ya hapa ni zaidi." Alimjibu Roberto.
"Nambie sasa kifuatacho maana uliniambia nikifika tu kuna jipya ni lipi hilo?" Titiana alimuuliza.
"Baada ya kuitrack namba ya Jackline jana usiku na leo kwenye mida ya saa tano niliibaini kuwa haiko mbali sana kutoka hapa Mbeya na nilipoiconvert kwenye mwendo nikaona ni kama masaa matatu hivi kwa mpiga gia mzuri na nilipomshirikisha dereva wangu akasema hiyo kazi ndogo sana kwake."
"Kwa hiyo tunaanza kuifuatilia?" Titiana alimuuliza.
"Kama kawaida mpenzi." Alimjibu.
"Okay sawa japo mwenzako nimechoka sana ila usijali." Titiana alikubaliana na matokeo safari ilianza kuelekea Makambako road.
"Suka mpaka hapo Makambako tutaingia saa ngapi maana hii ni saa kumi na nusu."
Roberto alimuuliza dereva.
"Hapo ongeza masaa matatu kamili."
Dereva alijibu huku akipangua mitaa ya makunguru kukwepa msongamano wa magari maeneo ya Mafiati mpaka Kabwe hivyo yeye aliingia njia ya kutokea Soweto. Maana anaufahamu msongamano wa Mbeya ulivyo unaweza poteza hata masaa mawili usipokuwa makini.
" Inaonekana wewe ni jeuri sana ee unaukimbia msongamano hapo mataa?"
Titiana alimuuliza dereva baada ya kuona anachepuka.
****
Baada ya kusubiri sana pale Ipogolo bila mafanikio yoyote waliona haina haja ya kuwafuatilia kule Makambako wakaona warudi Iringa mjini ndani ya TRAVETA HOTEL ambako walilala huku macho yao yakiwa kwenye system. Na kulipokucha asubuhi baada ya kupata kifungua kinywa na kuona bado system inaonesha wako ndani ya Makambako wakaona kuwa kwa hapo hakuna jinsi zaidi ya kuwafukuzia huko huko. Hivyo jet5 liliungurumishwa kushuka mteremko wa kuelekea Ipogolo kisha kuishika barabara kuu ya Dar - Mbeya.
"Wameshtukia nini? Mbona wanatukwepa sana hawa?" Aliuliza Jackline akiwa nyuma ya usukani.
"Hawana janja hiyo nahisi hapo walipo wanasubiria kitu na hata siku ambazo alipotea hewani nahisi ilikuwa mtandao au chaji tu na si vinginevyo."
Jessica aliwapa moyo wenzake huku jet likiendelea kukata mbuga na mabonde kuitafuta Makambako.
"Nina hamu nao hao hasa huyo anayejiita Jonathan? Nitahakikisha tunazipiga kavu kavu naye kabla ya kuanza kutenganisha viungo vyake." Jackline aliwaeleza wenzake atakachomfanyia baba yake mlezi.
"Endesha gari huko usije ishia kulia tu utakapomuona." Jasmine alimtania na wote wakacheka.
"Siwezi kubisha yote yanawezekana maana nina hasira sana na matokeo ya hasira hayanaga adabu eti." Jackline alimjibu
Hatimaye waliwasili mjini Makambako na kutafuta sehemu ambayo hawataweza kuipoteza signo na hivyo kutafuta Hotel ambayo iko karibu na barabarani hivyo wakakunja barabara kuelekea Songea road na kupaki nje ya hotel ya KIBADAMO hapo walichukua vyumba na kisha walipumzika kidogo. Lakini Jessica alitoa pendekezo kuwa wasikae vyumbani bali washuke chini na kutulia ndani ya gari ili iwe rahisi kuwakabili. Wakafanya hivyo na baada ya muda kidogo wakiwa ndani ya Honda jet5 waliona signo inatembea wakaanza kuifuatilia mpaka eneo la Majengo huko signo ikawaonesha kuwa wako karibu zaidi na maghala ya nafaka ikabidi waende maeneo yale kuangalia kama kuna nyumba ambayo itakuwa na gari ile ya Kluga. Walipaki gari lao karibu kidogo na Maghala na kisha kushuka na kuifuatilia.
Walizunguka kwa muda na kama bahati vile ndani ya nyumba moja waliiona ile gari ikiwa imepaki ndani yake wakaona isiwe shida wakarudi garini na kutulia hapo huku macho yakiwa kwenye kile kinjia cha kuingia mle ndani. Masaa yalipita lakini hakuna kilichotokea labda ile gari itatoka lakini wapi na hatimaye saa moja jioni iliwakuta wakiwa pale pale na kuamua kuondoka eneo lile kuhofia kushtukiwa na wenyeji wa maeneo yale hivyo wakapita na kwenda upande wa ambako walipaki lakini macho yakiwa pale pale.
"Mnaonaje gari tukalipaki barabarani kisha sisi turudi kwa mguu mpaka hapa na tukakae pale kwenye kile kiduka."
Jackline alitoa wazo na hivyo kuwaacha wenzake na kwenda kulipaki gari kando ya barabara ya Mbeya - Iringa kisha yeye akarejea kwa mguu kuungana na wenzake.
Ila kuna kitu kilimshtua kidogo kwani wakati akiwafuata wenzake aliiona gari ndogo taxi ikielekea pale pale walipo na kupaki nyuma kidogo ikiwa imezima taa.
Hapo ikabidi apunguze mwendo na kuanza kuivizia kujua wanatafuta nini eneo lile na kwanini watembee giza, akaona pia atoe simu kuwataarifu wenzake juu ya watu hao lakini simu hakuwa nayo alimuachia Jasmine aliyekuwa akiitumia kucheza gemu.
"Mungu wangu itakuwaje sasa?"
Jackline alijiuliza swali hilo baada ya kuikosa simu.
Akaona isiwe tabu akaanza kuwavizia mdogo mdogo na baada ya kuwakaribia akawaona watu wawili wakishuka kutoka kwenye gari hilo na kurudisha milango kisha kuanza kuelekea walikokuwa wakina Jasmine. Na kwa kuwa ilikuwa ni giza kutokana na kukatika kwa umeme hakuweza kuwaona vizuri hivyo ikabidi yeye alivizie hilo gari kuona kuna nini ndani yake. Alipofika kwenye ile gari alichungulia ndani na kumuona mtu ndani yake akaugonga mlango huku yeye akiwa kauficha mwili wake ubavuni mwa gari asionwe na mtu huyo aligonga tena ikabidi mtu yule ashushe kioo ili achungulie nje kuna nani aliyegonga gari. Alipochungulia na kuona hakuna mtu wakati huo Jackline akiwa amelizunguka gari ikabidi mtu yule ashuke chini kitendo cha kukanyaga tu ardhi alikutana na mdomo wa baridi wa bastola uliokuwa tayari kisogoni kwake.
"Tafadhali kwa usalama mkubwa weka mikono yako juu kabla sijakufanyia kitu mbaya."
Jackline alimuweka mtu kati kijana wa watu na kisha kumsogelea karibu zaidi ili kumtwanga maswali yatakayomuweka huru kijana huyo au kumchukulia uhai wake.
JE, NI NINI KITATOKEA?
USIKOSE KUSOMA HADITHI HII KATIKA SEHEMU ITAKAYOFUATA KUJUA KILICHOJIRI.
#SULTANUWEZO