IMETOSHA MAMA MKWE - 54 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 54

sultanuwezotz.blogspot.com 


Kuwasili kwa wazazi wangu nyumbani kwa mzee Nyaswa kuliwafanya hawa wazee kufurahi sana kwa kuwa toka wanifahamu mimi hawakuwahi kuwajua wazazi wangu zaidi ya kuwasimulia tu. Mzee Mbogo ambaye siku moja nyuma hali yake ilikuwa mbaya kutokana na kuupigania uhai wangu dhidi ya Bi Kiziwa na timu yake alikuwa anafuraha muda wote kiasi cha kumfanya Rachel aliyekuwa akiandaa moto kumuuliza.

"Babu nakuona una furaha sana kulikoni?"

"Unauliza mjukuu wangu? Huoni kuna nini leo?" Alimuuliza Rachel.

"Ndiyo nauliza inawezekana kuna dodo umeliokota pasipo kujua wengine hapa."

"Hapana mjukuu wangu, kinachonipa furaha leo ni ujio wa wazazi wa dada yako Tina, kumbuka kuwa siku zote tulikuwa naye kama mtoto asiye na kwao vile kumbe wazazi wapo na wenye nguvu kabisa."

"Ni kweli babu." Alimjibu. Wakati Rachel akiongea na babu mzee Mbogo sisi tulikuwa ndani ya kijumba cha msonge kilichojengwa kiasili mita chache kutoka nyumba kubwa ilipo tukiwa kwenye mazungumzo na mzee Nyaswa.

"Unajua wengi huamini kuwa tiba za asili ni uchawi hivyo huwa hawako tayari kupokea tiba hizi. Kiuhalisia ni kweli kwani asilimia kubwa uchawi umezaliwa kutoka kwenye mizizi hii hii tunayoitumia kwenye tiba." Mzee Nyaswa aliongea kwa kirefu kidogo.

"Ni kweli mzee Nyaswa kwani hata sisi hatuamini kwenye mizizi kutokana na imani zetu za kikristo." Baba alimwambia.

"Na ndiyo maana hatukuweza kumfanyia tiba za kina mtoto wenu Christina kutokana na tatizo lake na ndiyo maana tukaamua kuomba mfike tuwajulishe hili ili ninyi mfanye maamuzi juu ya Tina. Iko hivi, pamoja na mtoto wenu kuandamwa na matatizo tulijaribu kuyafuatilia kwa kina pasipo kumwambia Tina na tulichokipata ni kitu kingine kabisa."

"Kitu gani hicho mzee wangu?" Mama alimuuliza mzee Nyaswa.

"Mtoto wenu ana tatizo kubwa sana ambalo limetoka upande wako mama." Mzee Mbogo alifika na kulijibu swali la mama.

"Upande wangu mimi? Kivipi?" Mama aliuliza swali huku nasi tukibaki kujiuliza swali hilo hilo iweje upande wa mama uhusishwe na matatizo yangu na isiwe wakina Jofrey.

"Kuna jina la kiasili ambalo mlimpatia Christina...."

"Jina gani hilo? Kaundime?" Baba aliuliza.

"Hilo hilo... Mnajua mwenye jina hilo alikuwa mtu wa aina gani?" Mzee Nyaswa aliwauliza.

"Katika hali ya kawaida ni jina la kawaida tu ambalo tulimpa mtoto wetu kama kumbukumbu kwa mpendwa wetu tofauti na hapo hatujui ikoje." Mama alimjibu.

"Ilipofika muda wa kumbatiza mliamua kuachana na jina hilo la Kaundime na kumpa jina la Christina si ndiyo?" Mzee Nyaswa aliuliza.

"Ni kweli kabisa mzee wangu." Baba alimjibu.

"Sababu ilikuwa ni nini ya kufanya hivyo?" Mzee Nyaswa aliuliza.

"Tulifanya hivyo baada ya kushauriwa na wazee wa kanisa kitu ambacho tulikubaliana nacho na ndivyo ilivyokuwa." Baba alimjibu. 

"Na hapo ndipo yalipoanza matatizo kwa Christina ikianzia na kukatisha masomo baada ya kupata ujauzito...." Mzee Nyaswa aliwajibu. 

"Mhh kwa sababu gani sasa?" Mama kama hakuelewa hivi akauliza. 

"Marehemu mama yako alichukia sana baada ya kushushiwa heshima yake na kwa kuonesha hasira zake wazi aliamua kuanza kumuadhibu Christina." 

"Kuna ukweli wowote?" Mama aliuliza. 

"Na kama hivyo ndivyo ilivyo na wakina Jofrey waliingiaje?" Nilimuuliza. 

"Ni hivi katika Ulimwengu wa giza mawakala hutafuta upenyo kwa mtu waliyemtageti na wakiupata tu huanza mambo yao kwa urahisi kabisa." Mzee Mbogo alitujibu. 

"Kwa hiyo tufanyaje ili kulimaliza hili na ukizingatia sisi upande huu hatuuamini sana lakini kwa ajili ya mtoto wetu tutaufanyia kazi ushauri wenu." Baba aliomba ushauri baada ya kuelezwa kila kitu. 

"Na sisi hatupendi muende kinyume na imani yenu, hivyo mnachotakiwa kukifanya ni kurudi tu kanisani kumfanyia maombi atapona lakini pia mnatakiwa kurudi pale alipolala Bi Kaundime na kumuomba msamaha kwa kuandaa tambiko ambalo mtawashirikisha wazee wenu upande wa kikeni hata kama ninyi hamtashiriki lakini lifanyiwe kazi msipokuwa makini mtampoteza huyu." Mzee Mbogo aliwaeleza ukweli. 

" Tunashukuru sana wazee wetu kwa kutueleza chanzo cha tatizo la mtoto wetu na kama hamtojali sana tulikuwa na ombi kwenu."Mama aliongea.

"Ombi gani hilo?" Mzee Mbogo aliuliza.

"Kwa kuwa mmelitambua hili na ninyi ndiyo mlianza naye kuanzia mwanzo mpaka sasa hivyo tulikuwa tunaomba kama kuna uwezekano wa kumtibu hili tatizo na kumzuia mama mtusaidie." Mama aliona afunguke.

"Kwetu hakuna linaloshindikana hata kidogo na kwa kuwa mmetuamini tuko tayari kumsaidia binti yenu nafikiri hata yeye anakumbuka tuliwahi kumwambia kuwa tutampigania mpaka mwisho hata kama itatugharimu uhai wetu." Mzee Nyaswa alisisitiza.

"Tunawashukuru sana wazee wetu kwa msaada wenu na pili kwa kukubali kuwa ndugu zetu kwa kumruhuru Rachel kuwa sehemu ya wanetu hilo tu kwetu ni zawadi kubwa sana hivyo tunaomba mtuambie ni kiasi tukiandae kwa tatizo hili."

"Ha ha ha mnataka tuwatajie gharama mtaiweza?" Mzee Mbogo aliuliza.

"Tul...tuli...tulikuwa tunataka kujua tu." Mama alijibu kwa wasiwasi baada ya kumuona mzee Nyaswa kabadilika ghafla baada ya kusikia habari za malipo.

"Sikilizeni, Tina tutamfanyia tiba bure kabisa kwani kama mlivyosema ninyi wenyewe kuwa sisi tushakuwa ndugu sasa malipo yanatokea wapi la msingi mtakalotakiwa kulifanya ni kuandaa kuku wawili tetea wa rangi nyeupe pamoja na kitambaa kimoja cheupe na sarafu ya shilingi moja ya nyerere kazi itakuwa imekwisha."Mzee Mbogo alitoa maelekezo kwa wazazi wangu ambao walilipokea hili na kuahidi kulifanyia kazi siku iliyofuata kwa kuwa muda huu tayari ilikuwa ni usiku vitu visingepatikana kwa urahisi.

" Wewe Rachel hicho chakula hakiivi tu?" Mzee Mbogo aliuliza baada ya kuona kimya.

"Kiko tayari muda mrefu sana nilikuwa nawasubiri mmalize kwanza shughuli yenu." Rachel alijibu.

"Tumeshamaliza fanya maandalizi." Alimjibu.

"Wacha na mimi niende nikamsaidie." Niliongea.

"Na kweli mjukuu wangu kamsaidie tu maana huyo Rachel na jiko ni kama ardhi na mbingu vile japo kwa sasa toka amekuwa na wewe anajaribu." Mzee Mbogo alimjibu Tina. Wakati nikitoka mle kwenye kimsonge mara simu yangu iliita na nilipoangalia mpigaji ni nani kumbe alikuwa ni mwanangu Thobias haraka niliipokea.

" Shikamoo mama yangu." Alinisalimu.

" Marahaba mwanangu habari ya huko lakini? "

" Huku ni kwema mama yangu vipi unaendeleaje? Kwanini huniambii mpaka bibi aniambie au unaona bado mimi mdogo?"

"Hapana mwanangu wala si hivyo bali ni kuchanganyikiwa tu na bila shaka nafikiri ni kutokana na haya ninayopitia kwa sasa, nikuombe radhi kijana wangu kwa hili na nikuhakikishie kuwa nitakujulisha kila kitu nikiwa vizuri kwa sasa elewa tu kuwa mama yako niko nje ya mji nikihangaikia uzima."

"Nimekuelewa mama na mimi nikuhakikishie kuwa niko pamoja na wewe kwenye kila hatua yako na Mungu atatenda miujiza na yatapita tu."

"Amina mwanangu, nakupenda sana bila shaka hata wewe unalijua hilo."

"Nalitambua sana na ndiyo maana nilikupigia nijue kama kuna kosa nimelifanya mpaka usiniambie kuhusu hali yako." Aliongea kwa sauti ya kilio mwanangu.

"Siwezi kuwa mbali nawe mwanangu japo haya ninayoyapitia ni mapito tu mwanangu kuna siku yatakwisha tu na tutarudi kwenye maisha yetu."

"Sawa mama naomba nikuache upumzike ni usiku sasa ila kesho natarajia kuelekea jijini Mwanza kuonana na rafiki yangu Goodluck naomba ruhusa yako."

"Kuna nini huko mbona ghafla hivyo mwanangu?" Nilimuuliza.

"Kaniambia kuwa niende kule kuna dili anataka kunitengenezea."

"Kweli mwanangu?"

"Ndiyo mama kanihakikishia leo hii."

"Kama na wewe umeridhia hilo kwanini nikukatalie? Na babu yako je?"

"Kamanda tena kitambo sana nilishaongea naye na keshaniruhusu."

"Vizuri mwanangu nilitaka kushangaa yaani uondoke bila kuagana na wajina wako?"

"Isingewezekana mama."

"Basi tuwasiliane kesho ili nifanye chochote kwenye safari yako mwanangu."

"Usijali mama."

"Nikutakie usiku mwema maana nasubiriwa ndani."

"Na kwako pia mama yangu mpenzi." Niliagana na mwanangu baada ya maongezi ya muda mrefu na baada ya kukata simu kumbe Rachel alikuwa nyuma yangu akinisubiria nimalize kuongea na simu.

"Ukionaga simu ya mwanao unachanganyikiwa mwenyewe!!" Rachel alinitania akiwa kanishika mkono wangu.

"Ndiyo mwanangu wa pekee nifanyaje sasa?"

"Tuachane na hayo chakula kinapoa huku." Alinijibu tukiingia ndani ambako wakina mama walikuwa wameanza kula tulibakia sisi tu.


JE UNAFIKIRI NINI KITATOKEA KWENYE MWENDELEZO WA HADITHI HII?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post