IMETOSHA MAMA MKWE - 55
sultanuwezotz.blogspot.com
Wakati tukiendelea kula mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea kubwa likiwa ni namna gani zoezi langu litakamilika kwa wakati. Mzee Mbogo alitueleza kuwa usiku huu anataka afanye jambo ambalo litakuwa gumzo ndani mji wa Ilembula na Nyanda za Juu Kusini yote, baba alimuuliza anataka kufanya nini lakini mzee Mbogo hakuwa tayari kuweka wazi bali alichosisitiza ni kuwa tayari kupokea taarifa za kustaajabisha. Na kwa kuwa namfahamu mzee Mbogo kwenye kila jambo analosema nilijua fika kuna kitu kikubwa anataka kukifanya usiku huu.
"Hawawezi kuchezea akili zetu na kutuletea utoto wao sasa ngoja tuwaoneshe ukubwa wetu." Mzee Nyaswa naye alijazia. Nilimtazama usoni Rachel ambaye alikuwa akijilazimisha kuangalia lakini alikuwa kazidiwa na usingizi nikaona nimfanyie jambo nikapeleka mkono kwenye bakuli la maji na kisha nikamrushia matone usoni ndipo akashtuka na kusogea kwenye bakuli ambapo alinawa mikono na mimi nikainuka na kuondoa vyombo tulivyovitumia kwa chakula.
"Yaani huwezi amini dada usingizi ulikuwa unanichukua na kuniacha kumbe hata kunawa mikono nilisahau." Rachel aliniambia.
"Na ndiyo maana nikakunyasia maji usoni." Nilimjibu.
"Maneno ya babu umeyaelewa Rachel?" Nilimuuliza swali.
"Babu? Kasemaje kwani?" Aliniuliza.
Hapo nikagundua kuwa hakusikia chochote bali alikuwa amezama kwenye bahari ya usingizi ambapo nilimuokoa humo.
"Hakuna haja ya kukueleza wacha tufanye maandalizi ya sehemu za kulala."
"Ni kweli lakini hujaniambia alichokiongea babu."
"Mdogo wangu hakuna alichokisema nilitaka kuona kama ulikuwa nasi kumbe uliuchapa usingizi, hakuna jipya zaidi ya kuchimba mkwara tu." Nilimjibu.
"Okay sawa, wacha tuandae sehemu ya kulala wazazi kwanza maana wao ndiyo wageni." Rachel aliniambia tukitoka nje kwa ajili ya kufuata mikeka kwenye msonge ambao huhifadhi vitu mbalimbali vya mzee Nyaswa.
"Rachel nisubirini kwanza." Mzee Nyaswa alimwita Rachel kumbe alikuwa anatufuata nyuma,hivyo tulisimama kumngoja.
"Mnakwenda wapi?" Alituuliza.
"Tunafuata vilalio tuwatandikie wageni." Rachel alimjibu.
"Oohh sikuwajulisha kwenye hilo wageni watalala kwa mama Kashumba nilishaongea naye na akanikubalia hivyo cha kufanya ni kuwaongoza tu huko." Alitueleza.
"Sawa babu." Rachel alimjibu.
Hivyo safari yetu iliishia pale tukarudi ndani huku mzee Nyaswa akiwa mbele yetu. Na baada ya kuingia tu aliwaambia wazazi wangu wakapumzike maana ni usiku.
"Ndugu zangu naomba mkapumzike maana usiku umekwenda sana." Mzee Nyaswa aliwaambia.
"Tunashukuru sana mzee wetu." Baba alimjibu.
"Bila shaka Mr Thobias, Rachel wasindikizeni wageni nilikowaelekeza." Alituambia. Tuliwaongoza mpaka kwa mama Kashumba ambaye anaishi mita chache kutoka hapa kwetu hivyo haikutuchukua muda mrefu kufika.
"Hodi, hodi....." Rachel alibisha hodi.
"Karibuni, aahh kumbe kuna ugeni? Karibuni ndani jamani." Mama Kashumba alitukaribisha akiuweka sawa mlango.
"Asante mama na samahani kwa kukuweka macho mpaka muda huu." Rachel alimtaka radhi mama Kashumba.
"Hapana Rachel usijali nilikuwa sijalala kuna kazi imeniweka macho mpaka sasa." Mama Kashumba alituondoa hofu.
"Karibuni wageni."
"Asante dada tumekaribia." Mama alimjibu tukiwa sebuleni. Na sisi hatukuona sababu ya kuendelea kuwepo pale tuliaga na kuondoka kutoa nafasi kwa mwenyeji wetu kuwa huru na wageni wake.
"Mzee Nyaswa kiboko kumbe alishafanya maandalizi muda mrefu kiasi hicho?" Nilimwambia Rachel.
"Kwanini asubiri wakati akijua hana nafasi ya kutosha kundi kubwa la watu? Hata hivyo nasikia mama Kashumba ni mchepuko wake."
"Weee kweli?" Nilimuuliza.
"Acha kushangaa dada ni siri nakuibia hiyo." Alinijibu.
"Makubwaaa..."
"Ndiyo hivyo." Alinijibu tukiwa tumekaribia nyumbani. Lakini katika hali ya kustaajabisha kulitokea mwanga mkali kutoka juu na kumulika uwanjani kisha ukapotea.
"Kuna nini tena?" Nilimuuliza Rachel nikiwa na hofu kwani mwanga ule ulisababisha giza nene mbele yetu.
"Sijui ni nini?" Rachel alinijibu akichuchumaa chini.
"Unataka kufanya nini mdogo wangu?" Nilimuuliza.
"Ngoja kwanza." Alinijibu kwa kifupi na kutulia kwa muda kisha aliinuka na kunishika mkono.
"Dada wabaya wako wamewasili tayari hivyo tunatakiwa kutulia hapa kwa muda." Aliniambia.
"Hivi hawachoki tu kunifuatilia mtoto wa watu?"
"Wachoke wamefamikiwa wanachokitaka kwako?" Rachel alinijibu.
"Sas......" Kabla sijamalizia kile nilichotaka kumwambia Rachel ule mwanga ulirudi tena na safari hii ni kama kuna vitu vilianguka maana kulisikika kishindo kikubwa.
"Rachel Rachel unaonekana una huruma sana eee? Unanufaika kitu gani kwa mtu asiye ndugu yako kiasi cha kuacha kazi?" Ilisikika sauti ya Bi Kiziwa nyuma yetu ila safari hii ilikuwa yenye mtetemo mkubwa na yenye kutisha.
"Ni nani wewe?" Rachel alimuuliza.
"Hata nikikuambia haitasaidia kitu cha msingi nikabidhi huyo ndugu yako niondoke kabla sijafanya kitu kibaya kwenu." Bi Kiziwa aliendelea kutishia.
"Unasemaje wewe?" Rachel alimuuliza akigeuka kumtazama huku na kule japo hakuweza kumuona muongeaji.
"Umesikia tayari, maswali ya......" Kabla hajamaliza kuna mlio ulisikika upande ilikokuwa ikitokea sauti ya Bi Kiziwa na tulipogeuka huwezi kuamini tulikutana na sura za kutisha ambazo viwiliwili havikuonekana zilizokuwa zikipiga kelele kama mabundi na mafisi.
" Christinaaaaaaaaa njooooo.........." Ile mijitu ilianza kuita jina langu hali hii ilinitisha sana kiasi ambacho nilitamani kutimua mbio lakini Rachel hakuuachia mkono wangu. Kwa namna ya kipekee ambayo iliniacha mdomo wazi alitokea mzee Nyaswa akiwa sambamba na mzee Mbogo na kutua pale tulipokuwa kwa upepo mkali kiasi cha kusababisha upepo na vumbi kubwa japo ilikuwa ni usiku.
"Haya njooni mumchukue Tina huyu hapa...." Mzee Nyaswa aliongea na mwanga mkali ukatokea tena na hapo hapo tukawaona Bi Kiziwa, mama mkwe, wifi na Jofrey wakiwa wamevalia vipande vya kaniki nyeusi viunoni mwao huku wakina mama mkwe, Bi Kiziwa na wifi wakiziba na sehemu zao za maziwa pia huku mikononi wakiwa na vitu ambavyo sikuvielewa wala kuvijua.
"Si ninawaambia mbona hamuongei watawala?" Mzee Nyaswa aliwauliza tena lakini hakuna hata mmoja aliyemjibu.
"Kaa chini ni hatari dada." Rachel aliniambia kwa sauti ya chini, sikuwa na la kufanya muda huo zaidi ya kutii kila agizo. Tukikaa chini kuna moto ulianza kuwaka kutoka upande waliokuwa wakina babu kwenda kwa kina Jofrey japo ulikuwa mkali sana lakini katikati yake walionekana wakina babu.
"Hapa leo hakuna atakayetoka salama maana hii nguvu waliyoitumia ni ya juu sana." Rachel aliniambia.
"Itakuwaje upande wetu Rachel?" Nilimuuliza.
"Ni salama tu kikubwa tusiondoke hapa mpaka nitakapokwambia." Alinijibu.
Lilikuwa ni tukio la kutisha sana usiku ule kwani kila walipotaka kukimbia walidhibitiwa.
"Msihangaike kuinua nyayo zenu hapa leo mmegusa sehemu mbaya, kule Mbeya mlifanikiwa mkaona haitoshi na leo mmekuja hapa naomba niwaambie kuwa mmefuata kifo." Mzee Mbogo aliongea akiurusha mshale wenye moto ambao ulimkuta Bi Kiziwa kifuani na kupiga kelele za maumivu.
" Aaahh mnafikiri mtaniweza?" Aliongea hayo akienda chini.
" Hatukuwezi Bi Kiziwa lakini majibu unayo tayari." Mzee Mbogo alimjibu.
Kwa kitendo cha Bi Kiziwa kuanguka chini kiliwapa hofu wakina Jofrey ambao walianza kupiga kelele za kuomba msamaha maana walijua zamu yao imewadia.
" Kijana wetu, mtumishi wa serikali, mume wa binti yetu lakini uliyepoteza mwelekeo na kuamua kuwekeza nguvu zako kwenye ushirikina unajisikiaje ukiwa mbele ya mkeo katika hali hiyo?" Mzee Nyaswa alimuuliza Jofrey.
"Wazee wangu naombeni huruma yenu pia Rachel na mke wangu Christina haikuwa akili yangu bali hawa wazazi wangu." Alijibu huku akipiga magoti.
"Weeee nani mkeo? Mimi sina uhusiano na jitu chawi mume wangu ninayemfahamu wala si mchawi kama wewe!!" Nilimjibu.
Na mzee Mbogo alichokifanya wakati huu aliinua usinga wake juu na kisha kuushusha chini kitu kilichopelekea wote kwenda chini na kusababisha giza nene.
" Dada twenzetu... "Rachel aliniambia, tuliinuka na kuondoka haraka eneo hilo na kukimbilia ndani.
" Rachel mbona hivi?"Nilimuuliza.
" Utajua tu ikifika asubuhi." Alinijibu.
" Naombeni mkalale tuna masaa machache kuelekea asubuhi." Mzee Nyaswa alituambia baada ya kuingia na kutukuta tunapiga domo sebuleni.
" Sawa babu." Rachel alimjibu. Tuliingia chumbani kulala na kuwaacha wenyewe wakiendelea na ya kwao.
JE NI NINI KITATOKEA BAADA YA BI KIZIWA NA KUNDI LAKE KUNASWA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII TUJUE HATMA YA BI KIZIWA.
#SULTANUWEZO