IMETOSHA MAMA MKWE - 56 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 56

sultanuwezotz.blogspot.com 


Jogoo wa mtaa wa nyuma kama vile alihongwa siku hii ya leo maana siyo kwa makelele yake ya kuwika aliwika sana siku hii tofauti na siku nyingine, hakukuwa na sababu ya kuendelea kulala ilibidi tuamke na Rachel tayari kwa kuianza ratiba ya siku.

"Rachel nenda kawaamshe wazazi wenu kuna jambo tunataka kulijadili kabla ya kwenda kutafuta mnyama wa tambiko." Mzee Nyaswa alikuja na kumuamsha Rachel ambaye aliamka kitambo sana akichati tu.

"Sawa babu." Alimjibu.

"Fanya haraka kidogo." Alisisitiza mzee Nyaswa.

"Nimeshaamka.." Alimjibu akiinuka.

"Vipi?" Nilimuuliza.

" Unauliza wewe amka tu kumekucha." Alinijibu. Tuliamka na kuwakuta wamekaa sebuleni wakiteta jambo tuliwasalimu na kutoka nje.

"Sasa wewe nenda kawaamshe na mimi nikachote maji si unajua jana hayakubaki hata kidogo?"

"Si unisubiri tuongozane dada?"

"Hapana safari ya pili ndiyo tutakwenda pamoja wacha niwahi." Nilimjibu na kuelekea kilikokuwa kisima kinachotegemewa na kitongoji chote. Nikiwa njiani nilianza kuyafikiria mauzauza ya jana usiku namna yalivyotokea na yalivyothibitiwa. Niliogopa sana na kilichoendelea kunishangaza ni vile Rachel alivyokuwa jasiri kama vile mambo yale kwake ni kawaida tu.

"Rachel asipokuwa makini uganga wa mzee Mbogo unamsubiri shauri yake." Nilijisemesha mwenyewe nikiwa tayari kisimani na uzuri wake hakukuwa na foleni ambayo ingenichelewesha hivyo nilichota maji na kuondoka. Kwa mbali niliweza kusikia za watu wakiongea hivyo nilizungusha macho huku na kule kuangaza zinakotokea hizo sauti lakini sikuweza kuona ndipo nilipotega sikio vizuri nikawasikia kama vile kuna kitu kinafanyika ikabidi nitue ndoo nikajionee kwa macho yangu.

"Tobaaa...." Nilitokwa na neno hilo baada ya kuwaona watu ambao bila shaka hawakuwa wanandoa bali walikuwa wakichepuka vichakani wakiwa hawana hata wasiwasi wakiibomoa amri ya sita maana ilikuwa siyo kuivunja, nilirudi nyuma taratibu kabla hawajaniona nikaibeba ndoo yangu na kuondoka eneo hilo mpaka nyumbani ambako niliwakuta wakina mama wakiwa ndani wanajadili suala ambalo lilitokea usiku wa jana.

"Mzee Thobias.." Aliita mzee Mbogo.

"Naam mzee." Baba aliitika.

"Kama ambavyo mmesikia kutoka kwa mzee Nyaswa ndivyo ilivyokuwa na inawezekana tungekuwa legelege leo hii ingekuwa ni lugha nyingine kabisa." Babu Mbogo naye alijazia maelezo ya mzee Nyaswa.

"Sijui hata nishukuru vipi ndugu zangu lakini awali ya yote nawapa pole kwa kilichotokea."

"Nguvu na heshima ni kwa Mizimu yetu ambayo imeshikamana nasi kwa kipindi chote hiki pasipo kujali nani ni nani." Alimjibu mzee Mbogo.

"Kwa hiyo wako wapi hao mashetani?" Baba aliwauliza.

"Tumewafungia sehemu ambayo hawawezi kutoka hata wafanye nini."

"Tunaweza kuwaona?" Mama naye aliuliza.

"Dada Tina achana na hizo stori hebu twenzetu tukaongeze maji ili wakitoka kwenye kikao waoge na kupata kifungua kinywa." Alinishtua Rachel baada ya kunikuta nikiwa nimetegesha sikio karibu na mlango wa kuingilia sebuleni.

"Okay sawa twende." Nilimjibu nikimpokea ndoo moja kati ya mbili ambazo alizibeba mkononi. Tuliondoka na kuelekea bondeni kilipo kisima cha maji na njiani tukapishana na mama Kashumba akiwa na mzigo wa kuni kichwani.

"Nawaona wajukuu wa mzee Nyaswa."

"Ndiyo shikamoo..." Nilimsalimu.

"Hamjambo wanangu?"

"Hatujambo." Tulimjibu kwa pamoja.

"Haya ngoja niwaache niwawahi wageni wangu nyumbani."

"Sawa mama lakini walishaamka muda mrefu tumewaacha nyumbani." Rachel alimjibu.

"Maskini wameondoka na njaa... Niliondoka mapema nikijua nitawahi kurudi lakini ndiyo hivyo kuni zenyewe za shida shida."

"Usijali mama msaada uliowapa ni mkubwa sana tunakushukuru sana." Niliongea.

"Haya wanangu basi baadaye."

"Sawa mama." Nilimjibu huku nikimuonesha Rachel vumbi maeneo ya viwiko vya mikono,lakini Rachel hakuelewa chochote kile akabaki kanitumbulia macho yake tu kama vile kaishiwa muda wa maongezi kwenye simu ya muhimu. Tulipofika mbele kidogo ilibidi aulize tu.

" Mbona sikuelewa chochote pale?"

"Utaijuaje njia bila kuoneshwa?" Nilimjibu.

"Enhh lete habari..."

"Huwezi amini nilipokuja kuteka maji mwanzo si nimewafuma mama Kashumba akiwa sijui na mwanaume gani yule wakiusambaza mchanga." Nilimjulisha.

"Weeeee...! Hebu acha uongo wako dada asubuhi yote hii tena porini?" Alinibishia Rachel.

"Ni lazima ubishe hata mimi sikuamini hivyo hivyo nilivyosikia sauti zao mpaka pale nilipowasogelea karibu ndipo nilipopigwa butwaa."

"Unataka kusema kuwa huyu mama kafanya hivi baada ya kulaza wageni nyumbani kwake?" Rachel aliniuliza.

"Nahisi hivyo pia." Nilimjibu.

"Mhh kijijini kuna raha yake yaani watu wanajiachia tu kama vile mapori ni nyumba zao, aisee.." Rachel alijikuta akitokwa na maneno hayo. Tuliwahi kisimani tukachota maji na kurudi nyumbani haraka hapo kila mmoja alishika jukumu lake.

"Mbona mmechelewa hivyo au mlipotea nini?" Mzee Nyaswa alituuliza.

"Hapana babu ni kile kimuinuko ndiyo kilitupa changamoto kidogo." Nilimjibu.

"Haya fanyeni haraka tupate hiyo chai."

"Sawa babu dakika sifuri." Rachel alimjibu.

"Moto si uko tayari? Wewe kanunue vitafunwa na mimi wacha niishughulikie chai." Nilimwambia Rachel nikitoa hela kwenye pochi.

"Si ungeiacha hiyo hela mbona kubwa sana wakati hapa ninazo ndogo ndogo." Alinizuia.

"Hapana nimeshaitoa ipokee bwana tuulinde muda wasije toka chai bado." Nilimpa tahadhari.

"Sawa dada mkubwa nimekuelewa." Alinijibu akiipokea ile noti ya shilingi elfu kumi.

Baada ya chai tuliitwa nje na kuambiwa tulizunguke dimba ambalo lilikuwa limechorwa mbele yetu kwa unga.

"Hakikisha haukanyagi huo unga ni hatari." Mzee Mbogo alitutahadharisha.

Hivyo kila mmoja alichukua tahadhari kama ambavyo agizo lilisema. Kila mmoja alisimama sehemu ambayo alihisi ni salama kwake na kusubiri nini kilikuwa kinakwenda kutokea kwenye hilo dimba ambalo katikati yake kulikuwa na vyungu viwili vyeusi pamoja na vibuyu viwili vilivyokuwa na shanga nyeusi na nyeupe kwenye kishingo.

Alikuja mzee Nyaswa na kuingia katikati ya lile akiwa na mkia wake mkononi huku shuka jekundu likiwa limeufunika mwili wake.

"Tulikabidhiwa miti yote tuweze kuitumia kutatua matatizo yetu yanayotuandama huku jukumu likiwa limekwenda kwa wale waliopewa uwezo lakini miongoni mwetu tukabadili matumizi ya hii miti na kuamua kuitumia kuwadhulu wanyonge kwa lengo la kuzifurahisha nafsi zetu pasipo kuangalia madhara ambayo wenzetu watayapata." Mzee Nyaswa aliongea akiketi chini karibu kabisa na vilipokuwa vibuyu. Mzee Mbogo alitupa ishara na sisi ya kuketi huku yeye akiunyoosha juu mkono wake uliokuwa umekamata mkuki.

" Asanteni ndugu zangu kwa kujumuika pamoja nasi hapa ili kujionea yale ambayo tumekuwa tukipambana nayo kwa muda mrefu." Mzee Nyaswa aliendelea kuongea maneno yake ambayo maana yake haikuwa wazi.

Tukiwa tumekaa chini tukisubiri kuona kuna kitu gani kinakwenda kutokea mara mzee Mbogo alikuja kasi na kutupita mpaka ndani ya dimba ambako aliukita chini mkuki ambao aliukamata kisha akauachia.

"Mizimu ya mababu zetu kutoka kwenye koo zote za tuliojumuika pamoja kwenye kao hili tunawaalika mahali hapa muweze kuudhihirisha ukuu wenu hasa kwa wale wasiotii mamlaka." Aliongea mzee Mbogo na mzee Nyaswa yeye aliweza kuitikia tu.

"Karibuni, karibuni..."

Ghafla kulitokea giza nene ambalo lilitufanya kushindwa kuonana japo tulikuwa tumeketi karibu kabisa, na wakati giza hilo likiwa limechukua nafasi huku hofu ikiwa imetawala miongoni mwetu hasa mimi, mama na baba mara mwanga mkali ulitokea na kulimulika lile dimba tu, tukiwa bado tunashangaa tukio hilo kuna vitu vilianguka na kusababisha vumbi lililopelekea kutoona kitu pale kwenye dimba na vumbi lilipopungua na kuisha kabisa tulistaajabu kuwaona wakina Jofrey,nilishindwa kujizuia kabisa nilianza kulia kwa sauti kitu ambacho kilipelekea Rachel kunitoa eneo hilo na kuniingiza ndani ili kutoa nafasi shughuli iliyopangwa iendelee.

"Kwa kuwa mmevuka mipaka yenu na kuja kuvuruga amani ya sehemu hii jiandaeni kwa kupata adhabu sababu si mara yenu ya kwanza kufanya kosa kama hili. Hivyo jiandaeni kwa hilo." Mzee Mbogo aliongea akiwa kaunyoosha mkono juu wenye mkia huku mzee Nyaswa akiwa kasimama kibuyu kimoja mkononi akiwanyasia maji yaliyo kwenye kibuyu kwa kutumia ule mkia sijui wa Mnyama gani na bila shaka yale maji ni dawa kwani ilikuwa kila ikimfikia mhusika alikuwa akianguka chini. Tuliweza kulishuhudia tukio hilo tukiwa mlangoni na Rachel ambaye alikuwa amenishika mkono.

"Kiama cha wakina Bi Kiziwa kimefika hili ni tukio kubwa sana na huwa linatumia nguvu nyingi sana ambazo wakina babu wakifanya mzaha tu wanaweza hata kufa. Rachel aliniambia.

" Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa wanataka kuwaua?" Nilimuuliza.

" Huruma imekuingia eee?"

"Hapana nataka kujua tu." Nilimjibu.

"Kuwaua hawawezi lakini kitakachowapata ni kutolewa uchawi wao kwa kutumia ile dawa iliyo kwenye kile chungu na kibuyu cha kulia." Alinijibu Rachel. Mara lile giza lilitoweka na mwanga wa kawaida ukachukua nafasi yake na kuwafanya wote kuonekana vizuri kituko kilikuwa kwa Bi Kiziwa ambaye alikuwa maziwa nje kabisa akiwa kaficha nyeti zake kama ilivyokuwa kwa Jofrey lakini wakiwa hawajitambui kabisa kutokana na kunyasiwa ile dawa ambayo iliwatupa chini. 

"Amka, amka, amkeniiiiii......" Mzee Mbogo alipiga kelele ambazo ziliwazindua pale chini na kuamka. Waliduwaa baada ya fahamu kuwarejea kwani walishangaa kutuona tukiwa tumewazunguka. 


JE UNAFIKIRI NINI KINAKWENDA KUTOKEA? 


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI TAMU. 


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post