NITAKUUA MWENYEWE - 64 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 64

sultanuwezotz.blogspot.com 


Kwa kujitetea ilibidi aeleze anachokijua mpaka hapo alipo muda ule.

"Dada yangu usiniue nitakwambia kila kitu ninachokijua." Alianza dereva.

"Haraka nakusikiliza kabla ubongo wako haujawa halali yangu." Jackline aliongeza mkwara.

"Mimi ni dereva Taxi tu kutoka mkoani Mbeya, nimekodiwa tu hao wageni waliotokea sijui Brazil? Kwa maelezo yao."

"Brazil? Ina maana ni Roberto?"

Jackline alishangaa kusikia wageni kutoka Brazil hivyo hakutaka kusubiri haraka sana alimtaka wafuatane kule walikoelekea wale wageni.

"Si kweli aise hebu ongoza kuelekea kule walikoenda na ole wako iwe ni habari ya uongo utajuta kuisikia sauti hii."

Waliondoka na kuelekea kule walikoelekea wageni wa yule dereva Taxi. Walitembea na kuwakuta wakiwa wamekaa pamoja wakipiga stori kitendo kilichomfanya aamini na kufikia hatua ya kumsukuma pembeni yule dereva na kukimbia huku akiita.

" Robertoooooo........."

Roberto naye baada ya kuisikia sauti hiyo naye aliinuka na kumfuata Jackline.

"My sister Jeyiiiiiiiiiiiiii....."

Walipofikiana walirukiana na kukumbatiana kitendo kilichowapeleka mpaka chini.

"Kwanini umetufanyia hivi lakini Roberto?"

Jackline alimuuliza huku wakisogea pale walipokuwa wenzao.

"Nilitaka kuwaonesha mimi ni mtu wa namna gani?"

Roberto alijibu kwa kujiamini zaidi cheko likiwa limetawala uso wake.

"Njia uliyotumia ni nzuri lakini ni hatari sana kwani hapa tuko windoni na ninyi mmetokea unafikiri nini kingetokea mdogo wangu?" Jackline alimuuliza Roberto.

"Surprise zina sehemu zake Roberto shauri yako."

Jessica aliingiza neno lake naye na kama bahati vile umeme nao ulirejea kama kawaida.

"Jamani eee dogo lenu limetua ni kosa limefanyika lakini lengo langu limetimia kikubwa ni kujua mnatafuta nini hapa maana si kwa baridi hii." Roberto aliomba msamaha kiaina na kuuliza kilichowaweka pale.

"Hapa ndipo kazi yetu iliyotuleta Tanzania inapokwenda kuanzia kwani ndani ya jengo lile kuna gari ambayo ilimbeba mke wa Jonathan Ubao."

"Kwa hiyo mnataka kuniambia nimeuvaa mkenge kwa kufikia kazini?" Roberto aliuliza.

"Ni kweli kabisa Roberto karibu sana lakini hujaniambia uko na nani?" Jackline alijibu na kuuliza.

"Anaitwa Titiana Thompson ni mchumba halali wa kaka Roberto." Jessica alilijibu swali la Jackline.

"Waoo safi sana mdogo wangu, Titiana karibu mzigoni naitwa Jackline Kamanda wa kikosi nchini Tanzania."

Jackline aliwachekesha wenzake kwa namna alivyojitambulisha.

"Asante dada yangu nipeni jukumu langu nilifanyie mchakato mara moja."

Roberto tayari hakutaka kupoteza muda na stori ambazo zinaweza kuwapotezea windo lao.

"Kama tulivyosema kuna watu tunawavizia hivyo tuko hapa kwa staili ya fisi." Jasmine alimwambia Roberto.

"Sawa sawa ila naomba tuongozane na mmoja mpaka karibu zaidi na hiyo nyumba ili kujua tuanzia wapi kuliko kuwa hapa unajuaje kama wameshtukia mchezo na kuiacha system pale na wao kuishia zao?"

Roberto aliwapa neno ambalo liliwaingia vilivyo wakina Jackline. Hivyo haraka sana ikabidi waondoke wote kuelekea kwenye nyumba ile. Walifika mpaka pale wakiwa wote watano huku dereva akisalia kwenye gari. Na baada ya kufika pale kila mmoja alibana kwenye kona yake ili kutowapa nafasi wenyeji wa maeneo hayo kuwashtukia na hivyo kumfanya Roberto kusogea zaidi mpaka kwenye nyumba ile na kuchungulia ndani na baada ya kuona hakuna kitu cha kumsumbua akaamua kuruka ukuta na kutua ndani. Na kwa kuwa nyumba ile haina ulinzi wowote ikiwa ni ya mtu wa kawaida tu haikumpa changamoto sana kuweza kuingia ndani. Lakini akiwa kwenye nguzo ya nyumba ile mara alitoka mtu mmoja ambaye aliangalia huku na kule kisha akarudi tena ndani, kitendo kile kilimfanya Roberto kupata hamu ya kutaka kujua huko ndani kunafanyika vitu gani na ni wakina nani hao. Aliusogelea zaidi ukuta wa nyumba ile na kulikaribia dirisha ambalo ndani yake kulikuwa na sauti zilizokuwa kwenye mjadala ambao ulimvuta zaidi Roberto kusikiliza.

"Unajua nini jamani muda wa kuondoka unakaribia kwani hii ni saa tatu by saa nne tunatakiwa kuwa barabarani na tunakiwa kuingia njia ya Mtera to Dodoma kisha Mwanza lakini itatuchukua siku sita kutokana na kutafutwa kila kona."

 mmoja wao akizungumza hayo kitu kilichomfanya Roberto kuchungulia ndani kupitia dirisha na kubaini ni mtu mmoja mwenye minywele mirefu.

" Ila ninyi jamaa zangu maafande tutaachana hapa hapa kwa sababu tumeshamalizana tayari huko mbele mtajua wenyewe, lakini tu niwatahadharishe mkikamatwa kufeni kivyenu hakuna kumtaja mtu sijui kama hili mmelisikia?"

Aliendelea kuongea yule yule mwenye minywele mirefu.

" Huyu mtu mwenye minywele mirefu ni nani mbona anaonekana kusikilizwa zaidi?"

Roberto alijikuta akijiuliza swali hili na hivyo kuamua kuondoka hapo kwa kuruka ukuta na kutokomea zake kwa wenzake.

" Jamani kule ndani kuna kundi kubwa na bila shaka mpaka mzee Jonathan inawezekana akawa mle ndani kwani nimesikia wakitajwa maafande na pia kuna mtu mmoja mle ndani anasikilizwa sana hivi na ndiye alisema kuwa muda wa wao kuondoka ni saa nne na pia kuwataka wale maafande kuachana pale pale."

"Mhh yukoje huyo mtu kimuonekano?"

Jackline alimuuliza.

"Ni mtu mmoja mwenye minywele mirefu hivi ni kama Rasta."

"Ana Rasta? Hebu ngoja kwanza nifanye jambo moja hivi."

Pale pale Jackline alichukua simu yake kwa Jasmine na kuitafuta namba ya mkuu wa kituo cha polisi Makongolosi Afande Mkonge na kumpigia.

"Samahani mzee wangu hivi kwenye misheni zako umewahi kukutana na mtu ambaye ni Rasta?"

"Jackline uko wapi na kwanini umeuliza hivyo?"

"Nataka kujua tu mzee wangu sababu kuna ndoto huniijia ya mtu mwenye muonekano huo."

"Pole sana binti yangu huyo si mwingine bali ni mzee Jonathan alibadili muonekano wake ili kutoshtukiwa na vyombo vya dola."

"Asante mzee wangu." Jackline alikata simu yake na kuwataka waondoke sehemu hiyo na kurudi Hotelini kuchukua kilichochao na kuondoka zao. Walifika pale Hotelini kisha waliamua kumalizana na dereva wa Taxi kwa kumpa chake kisha waliingia ndani ya dude lao la Honda jet5 na kisha kutimua vumbi.

"Tunaanzia wapi kamanda wetu?"

Jasmine alimuuliza Jackline ambaye alisahau mpaka kuwajulisha wenzake alichoambiwa na mkuu wa kituo.

"Tunawatangulia mbele hawa watu, Jessica washa kifaa chako kisha tutawasubiri nje ya mji kidogo na watakapotukaribia tunaondoka ili kutowapa nafasi ya kutuona mpaka pale tutakapowatia mikononi mwetu, hamuwezi kuamini ndugu zangu huyo mwenye minywele ndiyo mzee Jonathan mwenyewe." Jackline aliwafafanulia wenzake.

" Kwa hiyo mtu wetu tunamkaribia kumtia mdomoni?" Jessica aliwauliza wenzake.

" Kama kawaida hana jeuri tena mzee Jonathan dakika zinahesabika." Jackline alimjibu.

Baada ya dakika kadhaa walifunga breki maeneo ya Iramba (Makambako) na kuwasubiri watu wao.

" Yote kwa yote Roberto tunakupa pole tena kwa kifo cha mama na ilikuwaje mpaka ikawa hivyo ilhali alianza kuwa fiti?"

Jasmine alimpa pole Roberto na kumtwisha swali.

"Asanteni dada zangu naelewa msiba huu wa mama ni wetu sote ila tu kuna ujumbe niliupata kutoka kwa Santana akijitapa kuwa amehusika."

Aliongea hivyo huku akiufungua  ujumbe ule na kuwaonesha wausome wenyewe.

"Kwa hiyo Santana aliamua kutupa kidonda kingine ee? Haina shida katupiga goli la kuongoza lakini ajue sisi ndiyo tutatwaa ubingwa."

Jasmine aliuliza na kutoa matokeo yake huku akijifuta machozi.

"Ni matarajio yangu kuwa ndani ya siku zisizopungua kumi tutakuwa ndani ya msitu wa Amazon tukizisaka roho zao. Kwa sasa ni zamu ya hili zee ambalo lina uhakika kuwa kutoroka kwake polisi baada ya kuhonga linajua limeshinda kumbe halijui nini kiko mbele yake."

Aliongea Jackline huku akisafisha kioo cha simu yake akiwa kaegemea usukani wa gari.

" Jackline jiandae signo iko nyuma yetu mita chache." Jessica alimpa taarifa Jackline.

Na kweli waliiona gari inakuja nyuma yao kwa kasi kitu kilichomfanya Jackline kulirudisha barabarani Honda lake na kuatamia njia huku macho yake yakiwa kwenye site mirror ili kuhakikisha hawaachi mbali watu hao.

" Mimi nafikiri tuondokane na utumwa huu, mnaonaje kama tukienda kuwasubiri pale njia panda ya kuingia Iringa mjini maeneo ya Ipogolo?" Jasmine alitoa wazo lake ambalo kila mmoja alikubaliana nalo hivyo kumfanya Jackline kukandamiza gia zaidi.

Waliwasili Ipogolo na kuipaki gari pembeni mwa barabara karibu zaidi na mchepuko wa kuelekea Iringa mjini. Na baada ya dakika kadhaa Kluga ilitia timu na kuingia sheli ambako ilikula mafuta ya kutosha na kuondoka tena na safari hii waliuanza muinuko wa kuingia mjini na kisha wakina Jackline nao wakaanza kuwafuata nyuma taratibu mpaka walipoifikia njia au barabara ya kuelekea Dodoma ambako gari lilishika kasi na nyuma yao wakina Jackline wakafanya hivyo hivyo.

Ndani ya gari la wakina mzee Jonathan stori ziliendelea kama kawaida huku wakiwa hawajui kama wanafuatiliwa nyuma na watu hatari ambao hawakati tamaa mapema kama wanajeshi wa Vietnam ambao ukiua kumi wanaongezeka hamsini.

"Nambie mke wangu.." Mzee Jonathan alimuuliza mke wake.

"Usingiza ulikuwa haupiti kwa kukuwaza mume wangu kipenzi."

"Tuko pamoja tena mke wangu na baada ya kufika Mwanza ni maandalizi ya safari ya kuelekea Uganda kuna sehemu nimeshapata jumba la kupanga nje kidogo ya mji wa Entebe huko tukifika tu kwa heri mkono wa sheria."

Mzee Jonathan alimtambia mke wake mipango ya baadaye ambayo alikuwa ana uhakika kama vile kaongea na Muumba wake.

" Ni kweli kabisa mume wangu tutatakiwa kufanya hivyo mapema kwani siku za hivi karibuni moyo wangu umekuwa ukinienda mbio sana wala hata sijui ni kwa ajili ya nini?"

"Ni kwa sababu ulikuwa mbali nami na sasa Ondoa shaka kidume wako nimekuja."

Lakini wakati wakiwa katikati ya maongezi kuna gari liliwapita kwa kasi na kwenda kusimama mbele kisha milango ilifunguliwa na kushuka watu wapatao watano wakiwa ndani ya maski huku mikononi wakikamata silaha.

" Mungu wangu kuna nini tena mume wangu?"

Mke wa mzee Jonathan alipatwa na mshangao uliomfanya kumuuliza mume wake ambaye walikuwa pamoja ndani ya gari moja.

"Wala hata sijui, bila shaka hawa ni Majambazi tu kwanini wavalie maski usoni wanaficha nini?"

Mzee Jonathan alijibu huku mwili wake ukiwa umetokwa na vipele vingi vya uoga kitu ambacho mke wake alikiona kitu hicho akajua kumekucha. Lakini wakati wao wakiulizana maswali yasiyo na majibu kijana mtukutu Masanja alifungua mlango na kujitupa kwa staili ya kuviringika kuelekea porini huku akimimina risasi kutoka kwenye moja bunduki ambazo mke wa mzee Jonathan alikuja nazo lakini ni kama alinyang'anya nyama kutoka mdomoni kwa simba mwenye njaa kwani alichokutana huko ulisikika mlio tu makelele ya maumivu na kisha alionekana mmoja akija mbele yao na kuwaonesha ishara ya kushuka chini huku mwingine akimfuata Masanja alikoingia.

"Mume wangu inakuwaje hapa?"

"Tujifanye wajinga tushuke tu kwani tukileta jeuri hapa yanatukuta ya Masanja."

Mzee Jonathan alimsihi mke wake kutii amri kabla ya kukutwa na makubwa. Mtu wa kwanza kutoka garini mikono ikiwa juu alikuwa ni dereva wao ambaye hakutaka kujiuliza mara mbili mbili. Mzee Jonathan na mke wake walifuata na wao wakifanya vile vile.

" Funga pingu hao fasta !!"

Jackline aliwaamuru wakina Jasmine kuwafunga pingu huku Roberto akiwa anakuja na Masanja ambaye alikuwa tayari kapoteza fahamu akiwa kambeba begani na kumpakia kwenye gari ile ile ya mzee Jonathan. Na baada ya kuwafunga na kuwafunga plasta midomoni waliwarudisha ndani ya Kluga na kisha Roberto alikaa nyuma ya usukani kisha magari yalikunja kona kurudi yalikotoka, kitendo hiki kilikuwa ni haraka sana na hakuna aliyepoteza muda. Mpaka yanafanyika haya si mzee Jonathan au mke wake aliyewatambua Watekaji wao.


SAFARI HII NI YA KUELEKEA WAPI?


USIHOFU, TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.


      #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post