NITAKUUA MWENYEWE - 65
sultanuwezotz.blogspot.com
Santana baada ya kufanikisha kumuua mama Roberto kupitia kwa Nesi Suzanne ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu walianza oparesheni ya kuisaka nyumba ya Roberto ili kumfungia kazi kabisa. Walihangaika kwa muda mrefu sana bila mafanikio yoyote ya kumpata. Hivyo kuamua kutuma timu ya watu wawili Robinson na Tom kuelekea nchini Namibia kuwasaka wakina Jackline na kuwatia nguvuni au kuwamaliza kabisa kwa kushirikiana na kikundi cha kihalifu kiitwacho 'The Black Eyez" kinachoongozwa na mwanamama Nafiwe kikiwa na maskani yake jijini Windhoek. Kundi hili limekuwa tishio sana ndani na nje ya Namibia kwa kufanya matukio ya kiporaji kwa kutumia Silaha na kufikia hatua ya kufungiwa misaada kutoka nje ya nchi kwenye mataifa makubwa kama Uingereza na Ujerumani kutokana na mauaji yalifanywa na kundi hili kwa kuwaua Watalii zaidi 20 kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo hayo mawili ambao walifika Namibia kwa shughuli za Kiutalii ndipo walipovamiwa na kundi hili na kuporwa kila kitu na kisha kuuawa. Lakini pamoja na harakati zote zilizofanywa na jeshi la Polisi la nchi hiyo la kuwakamata hazikufanikiwa kwani kwa mujibu wa habari za chini ya kapeti ni kwamba kundi hilo lina ushirika na baadhi ya viongozi wenye vyeo vya juu serikalini. Na ndiyo maana kila wanapojipanga kuwakamata taarifa zao huwafikia haraka 'The Black Eyez' na kuchukua tahadhari za haraka.
Robinson na Tom waliwasili nchini humo masaa ya magharibi kwa kutumia usafiri wa anga wakiwa na Jukumu moja tu la kuwasambaratisha wakina Jackline na kisha kurejea Brazil kuendelea na shughuli zao haramu.
"Karibuni sana vijana wa Santana Cruise katka ardhi ya watu weusi wenye roho za Kizungu kama sisi."
Nafiwe aliwakaribisha wageni wake muda huo wakiwa ndani ya gari kutoka Airport kuelekea nyumbani kwake.
"Asante sana madam." Alijibu Tom.
"Naitwa Madam Nafiwe maarufu kwa jina la Iron Lady' nikiwa ndiye Rais wa The Black Eyez' na Mfanyabiashara mkubwa sana hapa Namibia."
"Tunashukuru kukufahamu Madam, mimi naitwa Tom na mwenzangu hapa ni Robinson."
Tom naye alifanya utambulisho.
"Oohh jina kama la mwanangu wa kwanza Safi sana."
Aliwajibu wakina Tom.
"Jina gani hilo madam Tom au Robinson?"
Robinson aliuliza.
"Anaitwa Robinson na siyo Tom."
Aliwajibu Nafiwe.
Safari iliishia kwenye jengo moja la kifahari ambalo liko nje kidogo ya mji na kuingia moja kwa moja mpaka ndani na kupaki wakateremka na kukaribishwa ndani.
"Karibuni ndani wageni wangu."
"Asante sana."
Waliingia ndani na kupokelewa na dada wa kazi aliyekuwa kwenye maandalizi ya chakula cha jioni. Baada ya kuwakaribisha alirudi jikoni na kuelekea na mapishi.
"Jamani eehh hapa ndiyo nyumbani kwangu wenyewe wanasemaga Maskani na kama mjuavyo hapa ni kibabe tu hatulembi kwenye pazia jekundu pale ndiyo malalo yenu kwa siku mtakazokuwa hapa hivyo mnaweza kupeleka mabegi yenu kisha mengine yafuate."
Waliinuka na kupeleka mizigo yao chumbani huku mwenyeji wao madam Nafiwe akiingia chumbani kwake huku akilivua koti lake. Alibadilisha nguo zake na kurudi akiwa na katupia traki ya nyeupe yenye michirizi ya rangi ya bluu na tshirt nyeusi juu na kisha kurejea sebuleni ambapo aliwakuta wageniu wake wakiwa wanatazana Televisheni.
"Nilipewa taarifa zenu na dada yangu Nesi Suzanne kuwa siku za hivi karibuni utapokea ugeni kutoka kwa mtu tuliyemfanyia kazi pale hospitalini."
Alifungua mazungumzo madam Nafiwe.
"Ni kweli madam Uongozi umeamua kututuma huku Namibia baada ya watu ambao tulidhani kuwa tumewamaliza kumbe haikuwa hivyo waliweza kuokolewa na kisha kufanyiwa matibabu na sasa ni wazima wa afya. Mbaya zaidi wanaendelea kutekeleza mauaji yao kutokea huku wakimtumia kijana aitwaye Roberto ambaye tulikatisha uhai wa mama yake hivi karibuni kwa ushirikiano wako na dada yako Suzanne."
Alieleza Tom na kuinua glasi ya maji na kuipeleka mdomoni.
" Kwa hiyo mnataka kuniambia kuwa hao watu na timu yao wako hapa Namibia wakiendelea kuratibu mipango yao?"
Madam Nafiwe aliuliza.
" Ndivyo tunavyoamini madam."
"Labda tuichore ramani baada ya Mbwa wangu kufika baadaye kidogo kwani sikumbuki kama kuna kundi pinzani hapa."
"Madam tunakutegemea sana katika kulifanikisha hili kwani watu tunaokwenda kupambana nao ni hatari sana wana kila aina ya mbinu."
Robinson alimtahadharisha madam Nafiwe.
"Robinson umekwisha fika mikononi mwa Iron Lady hivyo shaka ondoa kabisa labda ninachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuongea na Bosi wenu Santana kila kitu kikae sawa kabla mtanange haujaanza."
Aliongea madam Nafiwe na kuiangalia namba ya Santana kwenye simu yake kisha kuipiga.
" The Iron lady." Alianza Santana baada ya kuipokea simu ya madam Nafiwe.
" Ndiyo mimi mwenyewe nambie kamanda wangu."
"Nakusikiliza wewe kwani ni matumaini yangu kuwa tayari timu yangu imewasili hapo kwani niliamua kuwasafirisha pasipo kufanya mawasiliano nawe kwanza nikiwa nimejazwa matumaini na dada yako Suzanne hivyo tunaweza kuongea sasa."
Alifafanua Santana.
"Nashukuru kwa kuniamini mimi na kundi langu nakuhakikishia asilimia mia ya kufanikisha jambo lako kikubwa ni mkwanja na si wa kitoto."
"Kama bei gani vile Iron Lady?"
Santana aliuliza.
"Mpaka unawatuma vijana wako kuja kwangu maana yake tayari ulishajipanga."
"Ni kweli lakini nitaanza na asilimia kumi na tano ya mkataba na kazi ikifanikiwa tu iliyobaki namalizia."
"Santana mimi ni tofauti na wengine, mara nyingi huwa nataka fedha zote mkononi kisha kazi ianze sababu natumia rasilimali watu, fedha na vifaa tukifeli zoezi na kila kitu kimesambaratishwa na maadui itakuwa hasara ya nani Santana? Ni kazi yangu mimi?"
Madam Nafiwe alifunguka.
" Okay tuachane na hayo nipe bei mara nifanye muamala leo hii hii ila tahadhari usipofanikisha tu umekwisha mdada."
Santana alimjibu.
" Sipigwi mkwara kihivyo Santana ulizoea kuwaonea hao hao hapa ni Himaya nyingine kabisa na kama una nguvu si ungekuja mwenyewe na ukileta za kuleta naanza na hawa kisha unafuata wewe, umenielewa?"
Nafiwe alimpakia Santana.
" Okay tuachane na hayo nipe bei."
Ilibidi Santana ashuke chini kiume.
" Nahitaji akaunti yangu isome kiasi cha shilingi milioni mia saba bila senti kisha kazi ianze leo leo."
"Hicho kiasi ni kikubwa sana Iron Lady."
"Yaani kwa sifa nilizoambiwa juu yako na umaarufu wako leo hii unalialia kama vile hujawahi fanya mishe za hivi?"
"Usininange hivyo wewe mwanamke, hela yako naingiza leo kabla ya jua kutua na kwa kukuonesha Santana ni nani naweka milioni mia saba na ishirini."
Madam Nafiwe alicheka sana baada ya kusikia majigambo ya Santana kisha akamjibu.
"Huo ndiyo umwamba Santana siyo unajilizaliza hapa."
Kisha alikata simu na kuingia ndani ambapo aliwaambia wakina Tom waoge kisha wapige msosi na baada ya hapo waingie matembezini kidogo mpaka usiku huko wanaweza pata pa kuanzia.
****
Waliwasili jijini Mbeya na kwenda moja kwa moja mpaka wilayani Chunya na kwa kuwa ilikuwa ni saa mbili ya asubuhi waliona wapumzike kwanza kwenye kona za mkoa eneo ambalo hutumiwa na Watalii mbalimbali kufurahia mandhari ya bonde la Usangu (View Area) na kupaki magari hapo huku mateka wao wakibakia ndani ya gari wakiwa bado kwenye sintofahamu ya wakina nani waliowateka.
"Vipi kwanini tunapaki hapa?"
Aliuliza Roberto baada ya kushuka kutoka kwenye gari.
"Kwa kuwa kumeshakucha inatubidi tuzuge hapa kwa masaa haya mpaka Magharibi ndipo tutaianza tena safari yetu kwani tuna kilometa mia na zaidi mbele."
Jackline alimjibu Roberto akiwa bado ndani ya Maski kitu ambacho ilikuwa ni ngumu kwa mzee Jonathan na mke wake kumtambua kutokana na kupungua mwili na kumfanya kuonekana mrefu na bado isingekuwa rahisi kwani siti ambazo walifungwa zilikuwa zimeteguliwa na kuwa kama zimelala vile.
"Jackline mkoa wa Mbeya una mandhari nzuri sana aise cheki hili eneo lilivyo utafikiri tuko Amerika au Afrika ya Kusini?"
Jasmine alilisifia eneo lile baada ya kushuka.
"Ni sehemu tu naambiwa ina maeneo mengi sana ya Kitalii ambayo hayajafikiwa bado wala kufanyiwa matangazo."
Jackline alimjibu Jasmine huku akiwa kamshikilia mkono Titiana na kusogea mbele karibu kabisa na kingo ya chuma ambapo bonde la Ufa linaonekana vizuri sana.
Aliipekua simu yake na kisha kupiga namba ambayo aliitaka.
" Shikamoo dada yangu."
Upande wa pili ulianza na salamu baada ya kupokea simu.
"Marahaba mdogo wangu, sasa nisikilize. Tuko huku Kona za Mkoa tunaelekea Lupa tukiwa na watu ambao huwezi kuwafikiria hata kidogo namaanisha kuwa mzee Jonathan pamoja na mke wake, tunawapeleka wapi haihusu kwa sasa mwambie Athuman akupe shilingi laki mbili au muongozane mpaka Supamaketi mkatununulie vyakula idadi yetu ni nane mjitahidi."
Jackline alimuagiza mdogo wake Shamimu.
" Makubwa, yaani mmemkamata mzee Jonathan?"
Shamimu alishangaa baada ya kusikia taarifa hizo.
" Kwani yeye ni nani mpaka tushindwe kumkamata?"
Jackline alimuuliza mdogo wake.
" Haya dada ngoja nikaongee na kaka Athuman juu ya hili ili tuje huko, na kaka si anaweza kuja pia?"
Shamimu alimuuliza Jackline.
"Ni yeye tu kikubwa tunahitaji vyakula msisahau maji na juisi pia msijisahau mkabeba na miwali maana mmekaa hapo Mbeya nina mashaka nanyi."
"Dada na wewe kwani sisi tumekuwa washamba kiasi hicho? Halafu pia matokeo yameshatoka dada."
Shamimu alimchomekea na ishu ya matokeo yake ya kidato cha nne.
"Fanya kwanza nililokuagiza tukilimaliza hili lillilo mbele yetu litakalofuata ni hilo la kwako na la kaka Athuman."
Jackline alimjibu Shamimu aliyeonekana mwenye furaha baada ya kutaja neno matokeo.
Baada ya kumaliza kuongea na simu alimgeukia Titiana na wakati huo Jasmine na Jessica walikuwa wakiwafuata na Roberto akibakia kama mlinzi pale kwenye magari.
" Umeona hili bonde linavyoonekana?"
Jackline alimuuliza Titiana akimshika begani.
"Vinyumba vinaonekana vidogo utafikiri hakuna watu wanaoishi huko?"
Titiana alimjibu Jackline na kuendelea kuyafurahia mazingira yale, kiuhalisia Titiana hakuwa muongeaji sana mara nyingi alionekana kuwa msikilizaji tu zaidi zaidi utamsikia akijibu tu maswali anayoulizwa na wenzake.
" Jackline wenzako tunatamani kama vile tuwashushe mle kwenye gari tuanze kuwasukumizia mijeledi ya maana ila basi tu."
Jessica alimwambia Jackline kile walichokuwa wakijadiliana na dada yake.
"Kuwa mpole Jessica hao ni wetu haraka za nini kwanza hapa ni barabarani si tutashangawa na wanaopita hapa tulipo ni salama kwani wao wanajua sisi ni Watalii kumbe tunaisubiri Magharibi ili tupite vizingiti vyote vya Polisi bila tabu yoyote."
Jackline aliwataka wenzake wasiwe na haraka kwani muda unakuja ambao kila mmoja ataifurahia show ya bure.
JE NINI KITATOKEA?
SEHEMU YA 66 INAKUSUBIRI KUPATA JIBU LA SWALI LAKO.
#SULTANUWEZO