NITAKUUA MWENYEWE - 77
sultanuwezotz.blogspot.com
"Mdogo wangu umeuaaa? Umemrahisishia kifo huyu mimi nilitaka afe taratibu kwa mateso makubwa ambayo yangemfanya ajutie kwa maovu aliyoyafanya ila ndiyo hivyo tena umeshindwa kuzuia hasira zako."
Jackline alimlaumu Roberto kwa alichomfanyia mtu ambaye walitegemea kumtumia kama daraja la kuwafikia wabaya wao.
" Dada Jackline nakuhakikishia kuwakamata hawa Washenzi mmoja baada ya mwingine kwa kutumia Weledi wangu lakini si kumtumia Nyang'ao mlaaniwa na kama nimewakosea naombeni mnisamehe lakini Roho yangu saafi kwa sasa japo bado waliokuwa nyuma yake."
Roberto alimjibu Jackline na kumhakikishia kuwa kazi ndiyo imeanza na ameahidi kuwanasa mmoja baada ya mwingine na katika hilo hakukuwa na la kufanya zaidi ya kuangalia mbele.
" Usihofu Roberto wala kujutia ulichofanya juu ya adui yako kwani hata ningekuwa mimi nisingevumilia hata kidogo kumuona adui mbele akivimba ilhali yeye mwenyewe kakiri kuhusika na mauaji ya mama. Pia tuliongea vile kwa kuangalia mafanikio ya haraka lakini kwa maneno yako tu tunaamini tutafikia tageti yetu."
Jasmine alimuondoa hofu Roberto na kumuahidi kushirikiana kwa kila kitu na hakuna haja ya kuleta mgawanyiko baina yao kisa tu hiki kilichotokea. Hivyo waliinuka na kukumbatiana pamoja kuashiria kuwa jeshi linaanza upya kisha Roberto na Titiana walikabidhiwa chakula wale huku wakina Jackline waliichukua miili ya wakina Dorine na dereva wake na kuipeleka kwenye kichaka kilichokuwa karibu na barabara kisha walirudi.
"Roberto mnaonaje muendelee kupata chakula garini huku tukipiga hatua mbele?"
Jackline aliwauliza wakina Roberto kama kuna uwezekano wa wao kupiga chakula kwenye gari ili sehemu hiyo waondoke mara moja.
"Why not?' inawezekana kabisa."
Alijibu Titiana na kuinuka kisha kumvuta mkono Roberto aliyekuwa bado kainamia chakula na kisha kuliendea gari. Waliingia na safari ilianza mara moja.
"Turudi Hotelini kwanza tukavute muda pale mpaka itakapofika usiku ndipo tuingie mtaani kuendelea na oparesheni yetu ya mtaa kwa mtaa."
Jackline aliwaelekeza wenzake wanaenda wapi muda huo. Kila mmoja alimuunga mkono na Jasmine alitoa pendekezo lake wakiwa pale Hotelini.
" Mnajua nini, tukifika pale inabidi turudi tena kwenye chumba cha mpuuzi Dorine tunaweza ambulia chochote na pia kama itawezekana itatubidi tukaonane na 'Operator Manager' wa kitengo cha Security tuweze kuzipitia zile CCTV Camera za chumba kile lazima tutapata pa kuanzia."
"Kweli kabisa hiyo yenyewe ila sijui kama watakubali kuturuhusu kuingia mimi nafikiri kuwa tunatakiwa kuharibu mfumo wa CCTV kama itatulazimu kufanya hivyo but nina uhakika kile chumba kitatupa majibu ya mahitaji yetu."
Jasmine aliunga mkono hoja ya Roberto lakini akatoa maoni yake yaliyopingana na Roberto. Waliwasili 'The Camel Hotel' na kuingia kwenye vyumba vyao na baada ya kuoga walikutana Restroom na kuanza kujadiliana ni kwa namna gani walianze zoezi lao kwani muda huo tayari ilikuwa ni Magharibi tayari.
Baada ya majadiliano hayo ndipo walikubaliana kuwa Roberto na Jasmine waende kwenye chumba cha Dorine huku Jackline, Jessica na Titiana wao waelekee Restaurant kuusoma mchezo kwa kila sura itakayokuwa mle ndani. Walitawanyika na kuelekea sehemu zao walizokubaliana. Baada ya kufungua mlango wa chumba namba 107 kwa kutumia funguo walizozichukua kwa Dorine ambaye tayari ni marehemu na kuingia ndani humo moja kwa moja walianza kukikagua chumba kile. Wakiwa wanakikagua kuna utofauti ambao waliuona mle ndani, kwanza kitandani kulikuwa na laptop ambayo inaonesha kuna mtu alikuwa akiitumia kwani haikuwa imefungwa pia ndani ya kabati kulikuwa na kimkoba cha kike ambacho baada ya kukikagua walipata hofu kidogo kama ni cha Dorine au kuna mtu mwingine ndani ya chumba hicho.
"Jasmine tutoke humu nahisi kuna mtu yuko ndani ya chumba hiki kutokana na mazingira ninayoyaona na kama sikosei anaweza kuwa katoka nje kwa muda."
Jasmine hakujibu kitu zaidi alimpa ishara ya kukikagua chumba kwanza kabla ya kutoka ndipo Roberto aliingia maliwatoni huku Jasmine aliangalia uvunguni na maeneo mengine ambayo alihisi anaweza kuona chochote lakini wote hawakuona chochote hivyo waliamua kutoka zao.
"Hapa tunatakiwa kubana sehemu tuchunguze ni nani alikuwa humu ndani."
Jasmine alimwambia Roberto huku akiufunga mlango.
"Ni kweli lakini pia ngoja nimpigie simu Jackline kumtaka awachunguze watu waliomo Restaurant."
Roberto alimjibu Jasmine.
"Okey fanya hivyo na mimi ngoja nikaifanye kazi yangu kwa mhudumu wa mapokezi."
Basi kila mmoja alifanya shughuli yake muda huo huku Roberto akimpigia simu Jackline.
"Dada Jackline chumba namba 107 kina mtu alikuwa mle ndani na ninahisi katoka mara moja hivyo jaribu kuwachunguza watu walio humo mlimo ninyi..."
"Hebu ngoja kwanza Roberto nakupigia sasa hivi."
Jackline alimkatisha Roberto baada ya kumuona dada mmoja ambaye alikuwa anakunywa juisi lakini baada ya kutazamana na Jackline dada huyo aliinuka na kutoka haraka nje ya Hotel na kuingia kwenye Taxi ambayo Jackline aliiona naye alikimbilia gari lao na kuanza kuifukuzia ile taxi. Na kwa kuwa giza lilikuwa limeanza kushika kasi haikuwa rahisi kwa watu waliokuwa ndani ya Taxi ile kujua kama nyuma yao kuna gari inawafuatilia. Taxi ile ilitembea na kutoka nje ya mji na kuelekea sehemu moja ambayo ni kama kijiji fulani hivi na huko gari liliingia ndani ya jengo moja lilionekana si la mtu wa mashaka kwani lilikuwa ni la kisasa zaidi na baada ya kufika dada yule alishuka akamlipa ujira wake kisha yeye akaingia zake ndani na geti likafungwa na ile taxi ikageuka na kuanza kurudi. Jackline akapiga hesabu akaona hakuna jinsi zaidi ya kumsimamisha dereva Taxi huyo hivyo akashuka na kuipiga mkono bila shaka gari ilisimama kabla dereva hajajua ashuke au ashushe kioo aongee na msimamishaji alishtukia tu mtu kashaingia ndani ya gari lake.
"Habari yako mpambanaji?"
Jackline alianza kwa kumsalimu dereva huyo.
"Nzuri dada yangu lakini mimi siyo mpambanaji."
"Hujanielewa maana yangu, mpambanaji ni yeyote anayepigania haki yake iwe ni chakula, uchumi au chochote kwa njia halali au siyo halali."
"Okay hapo mimi niko wapi?"
"Unataka uniambie kuwa kupitia hii Taxi huingizi chochote?"
Jackline alimtupia swali dereva huyo ambaye alionekana kuwa na mashaka hivi.
"Naingiza."
"Sasa hiyo ni nini?"
"Okay tuachane na hayo naomba nikusaidie dada yangu."
Dereva Taxi huyo alimkatisha Jackline ambapo alitaka kumsaidia.
"Huwezi kunisaidia wewe tatizo langu."
"Hee sasa kama siwezi kukusaidia kwanini umenisimamisha?"
Dereva huyo aliongea kwa kufoka kidogo kutokana na maneno ya kuudhi ya Jackline.
"Unaongea sana eee!!!"
Jackline aliongea hayo huku akiwa kaielekeza bastola yake sikioni kwa dereva Taxi huyo ambaye baada ya kuona kitu cha baridi kikigusa sikio lake alichanganyikiwa.
"Dada yangu kwa utani wewe umekubuhu aise."
"Unasemaje wewe?"
"Naomba unisamehe dada yangu."
"Naomba unisikilize vizuri mimi si mtu wa kawaida hata kidogo na ndiyo maana nimekufuata hapa bila wewe kujua. Wewe unafanya kazi na wahalifu huku ukijidai dereva Taxi."
"Hapana dada mimi ni dereva Taxi kabisa."
"Kelele !!!! yule uliyemleta huku ni nani na hii nyumba ni ya nani?"
"Hapo ni moja ya nyumba ya Tajiri mmoja mwanamke anayekimbiza kwa sasa hapa Namibia anaitwa Nafiwe."
"Ohhh vizuri unaweza kunikutanisha na huyu mfanyabiashara au ukanipa mawasiliano yake?"
Jackline alimuuliza dereva huyo.
"Huwezi kuonana na huyu Tajiri kirahisi hivyo."
"Okay vizuri naomba simu yako haraka."
Dereva huyo alitoa simu yake na kumkabidhi Jackline ambaye aliikagua na baada ya kukutana na majina ambayo aliyatilia mashaka aliiweka mfukoni kisha alimtaka ashuke garini huku naye akifanya hivyo baada ya kushuka.
"Haya changanya miguu haraka."
Kusikia hivyo tu dereva hakutaka kupoteza muda alianza mbio japo haikuwa bahati kwake kwani Jackline alimtandika risasi ya mgongo na kisha alirudi ndani ya gari na kuipiga namba ya Jessica.
"Jessica chukua bodaboda hapo njoo eneo moja hapa (huku akimulika kama ataona utambulisho wowote wa eneo hilo ndipo alikiona kibao kilichoandikwa 'White Color Supermarket'") kuna kibao cha 'White Color Supermarket' pembeni yake utanikuta."
****
Baada ya kupigwa na upepo wa kutosha Bi Elizabeth alipata fahamu na muda huu aliungana na familia yake sebuleni kutaka kujua ni nini kilimtokea Mustapha mpaka kufikia kutorudi nyumbani kwa muda wote huo.
"Mwanetu ulipatwa na nini mpaka kutoonekana kwa kipindi chote hiki?"
Mzee Jerome alimuuliza mtoto wake kwa niaba ya mke wake na Victor.
"Ni kweli kabisa kaka tuambie maana kuna kutoelewana humu ndani."
Victor alishindilia msumari kwenye swali la baba yao.
"Baba, mama na mdogo wangu Victor niweze kumshukuru aliyejuu kwa kuniweka hai mpaka leo hii, lakini kifupi ni kwamba nilitekwa na watu ambao wanawatafuta wakina Jackline."
"Unaona mume wangu si nilisema, si nilisemaaa? Yako wapi sasa yaani h....."
"Mke wangu hebu subiri amalizie kwanza hayo mengine ya nini?"
Mzee Jerome aliamua kumkatisha mke wake baada ya kuona anaingiza vitu vingine kabisa.
"Mwanangu endelea ikawaje?"
Mzee Jerome alimtaka Mustapha aendelee kusimulia mkasa wake.
"Hivyo baada ya dada yule ambaye aliniteka akiwa kama mteja wetu pale dukani kwetu alikwenda kunipeleka kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa kama sehemu ya kuhifadhia vyuma chakavu, alinifungia kwenye chumba kimojawapo na humo kulikuwa na kila aina ya uchafu huku kila siku asubuhi na jioni nikitandikwa bakora za maana huku maji yenye barafu yakimwagwa mwilini mwangu. Na waliniambia kuwa nikiwapa ushirikiano kwa kutaja uliko wewe baba na wakina Jackline ndipo wataniachia lakini kwa upande wangu sikuwa tayari kueleza hayo nilikuwa tayari kupoteza maisha baba. Kuna kipindi walikuja watu wengine hasa dada mmoja hivi ambaye sura yake si ngeni sana ambaye alikuwa akinipiga sana (huku akiwaonesha vidonda vilivyokuwa mgongoni na miguuni) kitu ambacho kilimfanya azidi kupoteza matumaini ya kuishi."
"Pole sana mwanangu yaani ulikuwa tayari kufa kuliko kuyataja mashetani?"
Bi Elizabeth aliendelea kuonesha chuki ya wazi kwa wakina Jackline.
"Mama hebu tulia basi mbona hivyo?"
Victor aliona mama yake kazidi akaamua kumtuliza.
"Mama kuna nini mbona naona kama kuna kitu kiko moyoni mwako?"
Mustapha alimuuliza mama yake.
"Hana lolote mama yako, unafiki tu na roho mbaya imemjaa hapo."
Mzee Jerome alimjibia kitu kilichomfanya asimame na kuondoka zake kuelekea chumbani kwake.
"Okay hivyo baada ya kuona kama hakuna mafanikio kwenye kunibana waliamua kubadilisha eneo la kunitunza bila shaka waliamua kutafuta sehemu ambayo hata wakiniua haitawapa tabu kunificha lakini hamuwezi amini Ukuu wa Mungu ulionekana pale kwani hata walikotokea sijui si wakanisaidia na kisha kunileta mpaka hapo nje kisha wao wakaondoka zao na nilipojaribu kuwataka waingie ndani walikataa wakaondoka zao."
"Pole sana mwanangu kwa yote uliyofanyiwa kikubwa Mungu kakuokoa kupitia kwa hao waliokuokoa ila hujasema ni wakina nani?"
Mzee Jerome alimpa pole na kisha kumtaka awataje ni wakina nani waliomuokoa.
"Si wengine bali ni wakina Jackline."
"Unasemaje Mustapha, wakina Jackline ndiyo waliokuokoa? Au umechanganyikiwa?"
Mzee Jerome hakuamini alichokisikia.
"Ndiyo hivyo baba, kwani hamjui kama wako hapa mjini?"
Mustapha alimtupia swali baba yake.
"Acha tu mwanangu wala sijui nisemeje juu ya hawa mabinti ambao mama yako hata kuwasikia hataki kabisa."
Mzee Jerome aliamua kufafanulia Mustapha.
"Wamekosa nini mpaka awachukie hivyo?"
"Tuachane na haya kikubwa umerudi tunamshukuru Mungu kwa hilo, hili la mama tuachane nalo watalimaliza wenyewe."
Mzee Jerome aliinuka na kumfuata mke wake ndani huku Mustapha na Victor nao wakibaki sebuleni kucheza games.
"Unawafahamu waliomuokoa mwanao?"
Mzee Jerome alimuuliza Bi Elizabeth baada ya kumkuta chumbani akiwa ananyoosha nguo zao.
"Hata nikijua itasaidia nini kwa upande wangu kikubwa mwanangu karudi salama nashukuru."
Bi Elizabeth alimjibu bila kumtazama usoni akiwa bize na nguo zake.
"Ila mke wangu una roho mbaya sana wewe maneno gani hayo? Na siku utakayojua kuwa maadui zako ndiyo waliomuokoa mwanao sijui utasema nini?"
Mzee Jerome Whistle aliongea hayo huku akiinuka na kutoka nje ya chumba hicho baada ya kuona hakuna ushirikiano wowote baina yake na mke wake.
" Sasa unakwenda wapi mume wangu si uniambie ni wakina nani hao?"
Bi Elizabeth alimkimbilia mume wake na kumshika mkono kumzuia kuendelea na safari akimtaka arejee chumbani amwambie ni wakina nani hao waliomuokoa Mustapha. Lakini mzee Jerome Whistle hakuwa tayari kurejea tena chumbani badala yake alimwambia kuwa mtoto wake atamwambia yeye anataka akapunge upepo nje, kitendo kilichomfanya Bi Elizabeth kuishiwa pozi na kurejea chumbani akiwa anajisugua vidole vya mikono huku macho yakiwa kwa mume wake aliyekuwa akiendelea kutoka akidhani atabadili mawazo.
JE, NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO