NITAKUUA MWENYEWE - 78 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 NITAKUUA MWENYEWE - 78

sultanuwezotz.blogspot.com 


Taarifa za kupatikana miili ya Dorine na dereva wake vichakani akiunganisha na tukio la mlinzi wake kupigwa kwa kumwagiwa mchanga machoni lilimchanganya zaidi Madam Nafiwe kiasi kwamba siku ya leo hakutaka kutoka kabisa nyumbani kwake.

"Ina maana hili kundi lisilo na jina limeshajua uwepo wetu kwenye misheni yao? Na kama siyo wao ni wakina nani hawa? Dogo Dorine ndiyo alikuwa na majibu yote ya hawa watu na kama siyo wao kwanini wamemuokoa yule kijana ambaye ilikuwa ndiyo tageti yetu ya kuwanasa?"

Madam Nafiwe alikuwa akijiuliza maswali yasiyo na majibu baada ya kusikia kuwa kuna miili imepatikana karibu na eneo ambalo gari lao lilishambuliwa. Alikata mafundo kadhaa ya maji huku akitembea tembea sebuleni kwake.

" Madam inakuwaje sasa?"

Tom alimuuliza baada ya kumkuta akihesabu hatua kama vile anahakiki ukubwa wa sebule yake ambayo siku zote huitumia yeye mwenyewe.

"Kuhusu nini Tom?"

Alimuuliza na yeye kama vile hakumsikia mwanzo.

"Unauliza tena kwani tulikuwa tunapitia taarifa gani kabla?"

"Si ilikuwa taarifa ya kuokotwa miili ya watu wetu kule porini?"

Madam Nafiwe alimjibu akiketi kitini.

"Na ndiyo maana nakuuliza iwapo kama kuna mpango mpya umeufikiria wa kuwakabili maadui."

"Siyo siri Tom unajua nini? Kazi hii niliiona ndogo sana ukilinganisha na vigongo ambavyo nimewahi kukutana navyo lakini kitendo cha kuuawa kwa Dorine ni dalili mbaya sana kwani kwa uimara wa Dorine lakini kathibitiwa ujue tuna kazi kubwa sana."

Nafiwe aliongea akiwa kasimama tena na kusogea mpaka dirishani ambako alikuwa sijui anaangalia nini nje.

" Wale madada ni moto mbaya madam ukiona Santana na jeuri yake yote kapaki na kuamua kukodi jeshi jingine ujue si mchezo."

Tom ndiyo alizidi kumchanganya kabisa Nafiwe.

"Kwa kauli hiyo unataka nikate tamaa?"

Nafiwe alimsogelea karibu Tom na kumuuliza swali la kibabe.

"Si maanishi hivyo bali ninachokitaka ni kujua tunaanzia wapi maana mpaka sasa maadui wametuotea na kupelekea watu wetu watatu kupoteza maisha huku wao wakipoteza wawili tu tena wa familia moja."

Tom bado aliendelea kumuelewesha madam Nafiwe ambaye moja wala mbili zilikuwa hazikai. 

" Tom nimepata wazo hapa hebu tumsubiri kwanza Asnat si unajua tulimtuma kule Hotelini akakichunguze chumba cha Dorine kuona kama kuna anaweza kupata chochote ambacho kiliachwa na marehemu kinachoweza kutusaidia kwenye zoezi letu."

Nafiwe alimwambia Tom wasubiri taarifa ya Asnat inaweza kuwasaidia. Wakiwa kwenye majadiliano mara simu ya Asnat iliingia na Nafiwe aliipokea. 

" Asnat kuna mpya yoyote ambayo umeipata huko?"

Madam hakusubiri mahubiri yaanze yeye alitaka kupata taarifa tu. 

"Madam hali ni tete sana maadui zetu wameshatapakaa kila sehemu kwani ukirusha hatua tu wako nyuma yako hivi ninavyokupigia simu tuko hapa nje ya ofisi kuna mwili wa dereva Taxi ambaye nimemtumia muda mchache uliopita unachunguzwa na askari baada ya kukutwa hapa huku wahusika wakiwa wametokomea na gari lake."

"Mhh hii kali hivi hawa watu ni majini au ni watu wa kawaida kwanini sasa? Mbona ishakuwa hatari kuna biashara kweli hapa mbona naona dalili za umauti mbele?" 

Madam Nafiwe anajikuta akiropoka tu baada ya kupata taarifa za kuuawa dereva aliyetumiwa na shushushu wake Asnat. 

" Lakini Bosi tumaini lipo kwani wakati nikiwa pale 'The Camel Hotel' kuna dada mmoja alikuwa anaongea na simu huku akinitazana sana kitu ambacho kilinifanya niondoke haraka pale na ndipo nilipochukua Taxi ambayo dereva wake kauawa hivyo moja kwa moja nahisi yule dada anaweza kuwa ndiye mhusika."

Asnat alimweleza Madam Nafiwe juu ya mtu ambaye alimuona Hotelini kuwa huenda akawa ndiye aliyehusika na tukio hilo. 

" Uliweza kuimaki sura yake ili tuingie mtaani kumtafuta ikiwezekana tuanzie mtego wetu pale pale hotelini."

"Sura yake sikuweza kuimaki kutokana muda wenyewe lakini kama lile eneo kalizoea tutamnasa tu na mimi bado sijaondoa vitu vyangu kwenye chumba cha marehemu Dorine kwani nilikuwa sijamaliza shughuli yangu nilitoka mara moja kupata chochote si ndiyo nikakutana na Mwanaharamu ikabidi nimpoteze maboya asijue niko wapi lakini alivyokuwa makini kumbe alicheza na akill yangu."

"Sasa hilo eneo halikuhusu waachie polisi wewe sogea karibu na hotel ili uweze kukutana na mtu ambaye mtasaidiana kulindana au polisi umewaeleza kuwa huyo mtu ulikuwa naye wewe?" 

"Hapana nifanye hivyo naumwa mimi wala na hata hivyo nimeshatoka hapo ndiyo nakaribia kufika Hotelini."

"Basi nampa namba yako ili akifika hapo mtawasiliana maana yeye si mwenyeji sana hapa mjini."

Baada ya maongezi ya muda kidogo waliachana na ndipo madam Nafiwe akamgeukia Tom na kumuelekeza cha kufanya kisha akamkabidhi namba ya simu na bila kupoteza muda Tom aliondoka zake. Huku nyuma baada ya Tom kuondoka tu simu ya Madam Nafiwe iliita lakini alipojaribu kuiangalia ile namba  hakuona kitu zaidi ya 'unknown caller' ikabidi apokee hivyo hivyo. 

"Nani mwenzangu?" 

Alianza kwa kuuliza swali. 

"Naongea na Nafiwe? Kiongozi wa kundi la 'The Black Eyez?" 

"Wewe ni nani?" 

Nafiwe alimuuliza tena mpigaji. 

"Jibu swali langu acha jeuri mwanamke."

Sauti ile ya upande pili iliendelea kumtia presha Madam Nafiwe. 

"Ndiyo mimi kuna nini na wewe ni nani?" 

Ilibidi akubali kisha naye akampiga swali. 

"Utanifahamu tu mimi ni nani siku nikija kwako kwani muda huu ninaoongea na wewe niko mlangoni kwako hapa."

Kusikia hivyo tu ni kama alishtuka hivi akatoka haraka kwenda getini huku akiangalia huku na kule kumuangalia aliyempigia simu yuko wapi na alipolifikia geti alichungulia kwanza kupitia matundu ya milango ya geti lakini hakuona kitu ikabidi afungue geti na kutoka nje, baada ya kufika nje aliishuhudia gari ikitimua vumbi kutoka eneo hili, ikabidi achukue simu na kutaka kuipiga ile namba lakini hakuweza kuiona ikabidi arudi ndani kwa hasira na kubamiza geti. 

"Ni nani huyu? Au tayari wameshapafahamu hapa? Mhh hapana hakai mtu hapa ngoja nitoke nikatembee kidogo washenzi hawa wasicheze na akili yangu mimi ndiyo Nafiwe Malkia wa The Black Eyez. Aliondoka zake mpaka mtaa wa pili lakini akaona apaki gari pembeni ampigie simu Santana kumjulisha juu ya hii hali inavyoendelea asikae tu huko Brazil akijua mambo yanakwenda kumbe hali tete.

"Mama la mama mwenyewe nambie."

Santana alipokea simu kwa mashamsham yote akiwa hajui kwanini kapigiwa.

"Nikwambie? Huku mambo si mambo wale watoto wa kike hawafai wamejitanua hao ni kundi kubwa hatari ni tofauti na nilivyotarajia mpaka sasa wametafuna watu wangu watatu wakati sisi tumewafumua wawili tu na wenyewe siyo wao ni wa kule hospitali yaani Daktari na mtoto wake."

"Unasemaje Kamanda wangu unamaanisha kazi imekushinda niingie mwenyewe kazini? Na vipi kati ya hao waliokufa vijana wangu wamo?"

"Kumbe huna akili wewe yaani unauliza watu tu si ndiyo? Sasa sikwambii kuhusu umenikwaza, kifupi kazi haijanishinda hata kidogo ila ninachotaka ni wewe kuja huku tuunganishe nguvu."

"Mungu wangu yaani kwa unavyoongea tu inaonesha fika umekata tamaa, Nisamehe kama nimekukwaza kwa kuulizia waliokufa kama ni wa kwangu ama wako please niambie nimefuta kauli ya mwanzo."

"Santa ee ni hivi, waliokufa mpaka sasa ni Afisa mipango wetu Dorine....." Kabla hajamaliza alikatishwa na Santana.

"Unasemaje Nafiwe? Suzanne kauawa? Usiniambie ndiyo tafadhali."

Santana alichanganyikiwa baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa Dorine (Suzanne).

"Nisikwambie vipi wakati tayari nishakupa taarifa Santa? Wengine ni dereva wake Dorine pamoja dereva Taxi aliyekuwa akitumiwa na kipanga wetu mtaalam wa IT Asnat."

"It's too much aisee kama hali ndiyo hiyo tunatakiwa kufanya kitu ama sivyo watatukalia kichwani hao."

"Na ndiyo maana nikaona nikupigie nikujulishe bro."

"Nimekupata ila endeleeni na michakato tutajua la kufanya."

"Poa poa bosi."

Baada ya kumaliza kuongea na Santana alikata simu na kisha akaliwasha gari na kuondoka zake lakini hesabu za kurudi nyumbani hakuwa nazo akanyoosha mguu.

"Uko wapi kiongozi wangu, yule dada tumemuona tena hapa lakini ametupotea sijui kaingia wapi?"

Ulikuwa ni ujumbe ambao uliingia kutoka kwa Asnat akimjulisha Madam Nafiwe kuwa kamuona tena Jackline pale 'The Camel Hotel' lakini hajafanikiwa kumuona kaelekea wapi.

" Msiondoke endeleeni kumchunguza maeneo hayo hayo anaweza kuwa kajificha tu na mimi niko njiani nakuja huko huko tuungane kumsaka mshenzi huyo mpaka kieleweke."

Alimjibu baada ya kuusoma ujumbe ule na kisha akaongeza kasi ili awahi kufika huko.

Kutokana na mwendo mkali aliokuwa nao ukichanganya na mawazo ya shughuli iliyokuwa mbele yake gari lilikwenda na kugonga kingo ya barabara na kuangukia mtaroni.

" Nini tena jamani mbona nakutana na majanga tena mimi, aghh mguu wanguuu ashiiiiiiii...." Akiwa anajichomoa kutoka kwenye gari ambalo lilikuwa limebondeka sana show ya mbele ilikuwa haitamaniki.

Alijivuta mpaka akachomoka na kusogea pembeni ambapo alikaa na kujifungua kitambaa kichwani ambacho alikitumia kujifutia damu iliyokuwa kwenye mguu wake wa kushoto pamoja kidole cha mguu wake wa kulia vilivyokuwa vinabubujika damu. Alijitahidi kuifuta na kisha akachana kipande cha kitambaa hicho na kujifunga kwenye goti sehemu ambayo ilionekana kuchubuka zaidi na alipomaliza aliinuka na kuondoka zake huku akiliacha gari lake lililokuwa halitamaniki kuliangalia tena kisha alitoa simu yake na kumpigia Asnat.

"Nakusikia Madam umefika?"

"Hapana nimepata ajali hapa karibia na hili daraja la kuchepuka kuja huko The Camel hivi niko mdogo mdogo nikiwa nakuja huko."

"Basi tulia hapo hapo nikufuate usije tonesha madonda yako."

"Okay basi fanya hivyo utanikuta njiani nikiwa nakuja taratibu Asnat."

Asnat alikata simu na kuchukua Taxi haraka iliyokuwa imepaki pale nje na kumuelekeza dereva wa taxi hiyo ni wapi wanatakiwa kuelekea na baada ya kuelewana safari ilianza mara moja. Gari lilishika kasi na kuifuata njia ambayo alielekezwa dereva lakini mambo yakawa tofauti kwani baada ya kumfikia tu Nafiwe gari lilimfuata na kutaka kumgonga ikabidi arukie pembeni kulikwepa na bila kusimama lilishika kasi pasipo kupunguza kasi hata kidogo.

"Weee mkaka huyo uliyetaka kumgonga ndiye tunayemfuata mbona unapitiliza tena?"

Asnat aliuliza akiwa kashika kichwa chake baada ya kuona mwendo si wa kawaida na dereva wa taxi hiyo alikuwa hamjibu chochote kile zaidi ya kuendelea kukanyaga mafuta.

"Ufanye chochote kile mrembo kama unayapenda maisha yako sijui umenielewa?"

Ilikuwa sauti nyororo na yenye kumaanisha kutoka siti ya nyuma ambayo ilimfikia vizuri sana Asnat huku kitu cha baridi kikimgusa kisogoni.

"Kuna nini jamani mbona sielewi wee kaka sinilikwambia kuna mtu tunamfuata kapata ajali mbona inakuwa hivi tena?"

Hakujali kama chuma kinacheza na kichwa chake yeye aligeuka na kumuuliza dereva ambaye hakuwa na habari naye zaidi ya kupambana kupishana na miti iliyokuwa ikirudi nyuma na kuufanya mpishano wa aina yake.

" Nimesema kimya na hutakiwi kufanya chochote mrembo kichwa kigumu eee nitakisambaza sasa hivi, kwanza nipe simu yako haraka."

Muda bastola ilikuwa ikikisuguasugua kisogo cha Asnat na kumfanya kuogopa sana pasipo na ubishi wowote ule aliitikia kwa kichwa na kuitoa ile simu na kumkabidhi Jackline kisha akamuamuru Roberto kuelekea kule kule kwa Gezra, hivyo hakukuwa na majadiliano zaidi kuelekea huko. Kwa ambaye angekutana na taxi hii kwa vyovyote angempa krediti kwa dereva huyu kutokana na mwendo wake na wengine wangekwenda mbele zaidi na kusema taxi hii imebeba magendo na ilikuwa ikifukuzana na maaskari wa kuzuia magendo.

"Shuka haraka wewe mrembo uliyeshindwa kuutumia uzuri wako kufanya kazi ambayo ingekuletea heshima kwa jamii na iwapo ungeenda mbali zaidi ungeweza hata kugombea Ulimbwende wa Dunia na bado taji hilo lingekuwa la kwako ila kwa kuwa ulichagua kufanya shughuli hii ngoja sisi tukuvishe taji la Umauti ambalo hutolivua maishani.

"Pa pa pa paaaaa................"

Ulikuwa ni mlio wa risasi mfululizo zilizosambaratisha kichwa cha Asnat ambaye aliangukia uwanja ule ule ambao uliyachukua maisha ya mlinzi aliyetaka kupambana na Roberto. Na baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa walipongezana kwa hatua waliyoifikia kisha waliingia garini.

"Roberto unafahamu kuwa kila hatua tunayoifikia tunakaribia ushindi?"

"Ni kweli kabisa Jackline na nina uhakika kwa mbinu hii watakufa kama kuku kama siyo panya."

Wakiwa wanaendelea kupongezana mara simu ya Asnat iliita.

"Asnat mbona kimya mpaka sasa hujaondoka tu au kuna lolote umefanikiwa kuliona? Na pia ni kama mkosi vile huwezi amini Asnat kuna taxi imepita hapa kwa mwendo mbaya sana almanusra nigongwe."

Nafiwe alijiachia akifikiri kuwa anaongea na Asnat kumbe simu ilikuwa sikioni kwa Jackline.

" Nafiwe, Nafiwe, Nafiwe huyo uliyefikiri kuwa ni Asnat umechelewa sana muda tayari anasalimiana na Dorine huko kuzimu muda wa wewe kuitwa Nafwa na siyo Nafiwe wala Nafiwa umewadia jiandae, mimi ndiyo kubwa la Maadui."

Alikata simu na kuitupa pale pale karibu na ulipo mwili wa Asnat na kumtaka Roberto aendeshe gari waondoke eneo hilo.

" Tukikaribia makazi ya watu simamisha gari tulitelekeze kisha tutatembea mpaka tupate usafiri wa kukodi."

"Sawa sawa Jackline."

Roberto alimjibu na kukanyaga mafuta kuelekea mjini.


JE, NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA YA NITAKUUA MWENYEWE.



       #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post